1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la amani DRC

Benjamin Kasembe15 Februari 2019

Tamasha la amani litakalohudhuriwa na zaidi ya watu 30,000 kutoka kote barani Afrika wakiwemo wasanii wa muziki limeanza Kivu Kaskazini nchini DRC.

https://p.dw.com/p/3DSTB
Lexxus Legal Peace one day Kongo
Picha: Getty Images/AFP/P.Moore

Kumeanzishwa rasmi Mkoani kivu kaskazini tamasha la amani litakalohudhuriwa na zaidi ya watu 30,000 kutoka kote barani Afrika wakiwemo wasanii wa muziki watakaotumbuiza kwa siku tatu mfululizo nyimbo za amani hadi keshokutwa Jumapili. 

Huku jeshi la Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo likiendelea kukabiliana na baadhi ya makundi ya waasi wanaopiga kambi katika misitu mkoani Kivu Kaskazini wasanii nyota ulimwenguni wamemiminika mjini Goma ili kutumbuizia katika tamasha hili la amani.

Akizungumza na DW bwana Dieudone MANGO afisa mawasiliano wa tamasha hilo amesema kwamba kwa muda wa siku tatu mfululizo watakaohudhuria watanufaika na kuhimizwa kuhusu amani kupitia muziki utakaotumbuizwa na nyota mbalimbai wa mziki kutoka barani Afrika.

Upande wa wakaazi wa mji huu wa Goma wanaonekana kutokuwa na muelekeo wa pamoja kuhusu tamasha hili la muziki linaloandaliwa kila mwezi wa Februari hapa mjini Goma kwa madai kwamba ni njia moja ya kukuza amani hapa mashariki mwa Congo kama inavyokuwa ikitamkwa na viongozi waandalizi wa tamasha la amani.

Tamasha la Amani kwa njia ya muziki huwavutia wasanii kutoka ndani na nje ya DRC
Tamasha la Amani kwa njia ya muziki huwavutia wasanii kutoka ndani na nje ya DRCPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Hata hiyo wakazi wengine waliokuwa tayari wamejipanga kwenye foleni kufuatia taratibu zilizoko, wamebainisha kuwa na furaha na kutoa wito kwa kila raia kudumisha amani kote katika nchi za ukanda wa maziwa makuu kwa manufaa ya maendeleo kote barani Afrika.

Tamasha hili la sita la amani litakalowashirikisha wanamuziki FALY IPUPA wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, YOUSUFA kutoka Ufaransa na vijana wasanii wengine kutoka nchi za ukanda huu wa maziwa makuu linafanyika wakati baadhi ya vijiji na wilaya mkoani Kivu Kaskazini zikikabiliwa na homa hatari ya Ebola.

Kupata amani ya kudumu bado kumesalia kuwa kitenda wili kwa mamia ya wakaazi wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya wanamgambo wanaomiliki silaha na kusababisha wengi wa wakaazi kuvihama vijiji vyao ili kupata hifadhi katika maeneo tulivu.