Tanzania, Kenya na Uganda zatinga fainali za Afcon
24 Machi 2019Timu ya taifa ya Tanzania ilifanikiwa kupata mabao 3-0 dhidi ya majirani zao wa Uganda katika mchezo ambao ulikuwa ni lazima Taifa Stars kushinda. Uganda imeshika nafasi ya kwanza katika kundi L, ambalo lilikuwa na timu za Uganda, Cape Verde, Lesotho na Tanzania. Kwa ushindi huo Tanzania inashika nafasi ya pili baada ya Uganda , baada ya mchezo kati ya Lesotho na Cape Verde kutoka sare bila ya kufungana.
Tanzania imetimiza pointi 8 , ikifuatiwa na Lesotho ambayo baada ya sare dhidi ya cape Verde itakuwa na pointi 6 tu.
Ni mara ya kwanza kwa Tanzania , Uganda na Kenya kutinga kwa pamoja katika fainali hizo za kombe la mataifa ya Afrika tangu kuanzishwa kwake.
Tanzania imewahi kushiriki katika fainali hizo miaka 38 iliyopita, lakini Uganda imewahi kushiriki mara mbili.
Kenya ilicheza na Ghana siku ya Jumamosi kutafuta nafasi ya kwanza ama ya pili katika kundi lake la F , ambapo mchezo wake mjini Nairobi ulimalizika kwa Ghana kujipatia ushindi wa bao 1-0.
Katika michezo ya leo timu ambazo zimefanikiwa kuingia katika fainali hizo za Afcon 2019 ni pamoja na DRCongo ambayo iliishinda Liberia kwa bao 1-0, na kuungana na Zimbabwe kufuzu kucheza katika fainali hizo. Zimbabwe iliishinda Congo Brazzaville kwa mabao 2-0.
Timu nyingine iliyofuzu ni Benin iliyoifunga Togo mabao 2-1 nyumbani. Togo inajiunga pamoja na Algeria katika fainali hizo. Afrika kusini na Libya zinapambana , ambapo Libya inalazimika kushinda, wakati Afrika kusini inahitaji sare kuweza kufuzu.