1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kuondoa marufuku ya uwindaji

23 Novemba 2018

Mpango wa serikali ya Tanzania kuondoa marufu dhidi ya uwindaji iliyowekwa miaka mitatu iliyopita. Nia ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kurejesha turaathi za Waafrika zilizoporwa wakati wa ukoloni.

https://p.dw.com/p/38meA
Tansania Selous Reservat
Picha: WWF Deutschland/Michael Poliza

Tunaanza na Gazeti la Frankurter Allgemaine la mjini Frankurt ambalo wiki hii limeandika juu ya mpango wa serikali ya Tanzania kuondoa marufuku ya Okotoba 2015 dhidi ya uwindaji wa wanyamapori kwa wenyeji, na kuweka maeneo makhususi ya uwindaji katika mikoya ya Manyara, Lindi, Tabora, Katavi, Singida na Pwani. Haya yalitangazwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori James Wakibara. Mbali na Watanzania, wageni wanaoishi nchini Tanazania watapatiwa vibali kuwinda kwa ajili ya kitoweo.

Wakibera alisema serikali inahitaji mapato yatokanayo na biashara ya uwindaji ili kulinda mazingira na spishi za wanyama. Eneo moja la uwindaji litakuwa linakodishwa kwa Dola za Marekani elfu 60 kwa mwaka. Frankfurter Allgemeine linanukuu gazeti la The East African, lililoripoti kwamba kuuwa tembo moja kutagharimu dola 15,000, huku simba akigharimu dola 12,000.

Tansania Selous Reservat
Mizoga ya tembo katika hifadhi ya wanyama ya Selous, kusini mwa Tanzania.Picha: WWF Deutschland/Green Renaissance

Tanzania ilipigia marufuku uwindaji kufutia vidio iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wawindaji wa Kiarabu waliovyokuwa wakitumia leseni yao kuuawa wanayama wadogo na wenye mimba kinyume cha sheria. Lakini wenyeji pia walipigwa marufuku kuwinda kwa hoja kwamba utoaji wa leseni za uwindaji ulikuwa unahamasisha ujangili.

Sensa ya wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2014 ilionyesha kuwa tembo 43,521  walikuwa wanaishi bado nchini humo kwa wakati huo, hiyo ikiwa ni pungufu ya karibu asilimia 60 ya idadi ya mwaka 2009 ambapo tembo 109 051 walirekodiwa. Licha ya kupungua pakubwa kwa idadi ya wanyama hao, gazeti la Frankurter Allgemeine linaripoti kuwa uwindaji una mashabiki wengi, hata miongoni mwa wahifadhi.

Makumbusho za Ufaransa kusalia tupu?

Rudisha kila kitu, ndiyo kilikuwa kichwa cha habari cha gazeti la Süddeutsche Zeitung, likiripoti juu ya hatua ya Ufaransa kutaka kurejesha turaathi za kitamaduni zilizoporwa barani Afrika wakati wa enzi za ukoloni. Mwanzoni mwa mwaka wa 2017 Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisababisha msisimuko alipoweka wazi matamshi ya watangulizi wake wote kuhusu ukoloni. "Ukoloni ni sehemu ya historia ya Ufaransa," alisema Macron, na kuongeza kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Novemba 28, akatoa ahadi kwa wanafunzi mjini Ouagadougou, Burkina Faso, kwamba katika kipindi cha miaka mitano yatawekwa mazingira ya urejeshaji wa kudumu au wa muda wa turathi zote za kitadamaduni za Waafrika zilizoko katika makumbusho za Ufaransa. "Urithi wa kitamaduni wa Afrika," aliongeza kupitia ukurasa wa Twitter, "hauwezi kuendelea kuwa mfungwa katika makumbusho za Ulaya."

2017/11/28. French President Macron Addresses Students in Ouagado
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alipozungumza na wanafunzi wa chuo kikuu cha Ki Zerbo, mjini Ouagadougou Novemba 28, 2017 na kuahidi kurejesha turaathi za Afrika zilizoko Ufaransa.Picha: picture-alliance/dpa/Ahmed Ouoba

Mwezi Machi mwaka huu, akawapa kazi mtaalamu wa historia Benedicte Savoy, anaefundisha Berlin na Paris, na mchumi wa Kisenegali Felwine Sarr, wote wakiwa na umri wa miaka 46, kuchunguza uwezekano na utaratibu wa kurejesha turaathi hizo. Walikwenda Benin, Senegal, Mali na Cameroon, wakaandaa warsha mjini Dakar na Paris, wakazungumza na wafanyakazi wa makumbusho, wanasayansi, mawakili na wanasiasa kutoka mataifa yaliokuwa makoloni na Ufaransa na nchini Ufaransa kwenyewe.

Na sasa, katika waraka wa kurasa 240 waliomkabidhi rais Macron siku ya Ijumaa, wanaeleeza kwa uwazi kabisaa nini kinapaswa kufanywa: Mara moja na bila uchunguzi mwingine, kila kitu kilichochukuliwa wakati wa hatua za kijeshi kirejeshwe, na kila kitu kilichochukuliwa kabla ya 1960 wakati Ufaransa ilipojitoa afrika, kinapaswa kurejeshwa.

Biashara kati ya Ujerumani na Afrika

Gazeti la Süddeutsce Zeitung linaagazia uwekezaji wa makampuni ya Ujerumani barani Afrika. Linasema makampuni ya Kijerumani yanayofanya biashara barani Afrika yanapaswa kuwatendea vyema watu pamoja na mazingira. Lakini linauliza je, nani atasimamia utekelezaji wa hili?

Kujibu hilo, gazeti la Süddeutsche lilifanya mahojiano na waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller, pamoja na mtaalamu wa maendeleo na biashara, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Boniface Mabanza.

Miongoni mwa mambo yaliojadiliwa ni pamoja mkakati wa ushirikiano kati ya Ujerumani na Afrika - maarufu Compact Africa, uwekezaji na haja ya kushughulikia changamoto za kisiasa zinazoyakabilia mataifa mengi ya Kiafrika. Mtaalamu wa maendeleo na biashara Boniface Mabanza, anaamini Afrika inaweza kupiga hatua kubwa iwapo matatizo yake ya kisiasa yatapatiwa ufumbuzi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/SZ, FA

Mhariri: Saumu Yusuf