TEPCO yakiri ajali ya Fukushima lilikuwa linazuilika
13 Oktoba 2012Hiyo ni mara ya kwanza kabisa kwa kampuni hiyo ya Tokyo Electric Power Company, TEPCO ambayo imelaumiwa kwa kujaribu kukwepa kuwajibika kutokana na balaa hilo baya zaidi la kinyuklia katika kipindi cha muda mrefu nchini Japan kutoa tamko la kukiri. Ripoti hiyo inasema kabla mawimbi makubwa hayajakishambulia kiwanda hicho mwezi Machi mwaka 2011, kampuni hiyo ilikuwa inafahamu kuwa vizuizi dhidi ya majanga asili vilikuwa havikidhi kiwango, lakini haikuchukua hatua kwa kuhofia madhara ambayo yangetokea.
Sababu za kutokuchukua hatua
"Kulikuwa na hofu kwamba kiwanda kingehitajika kufungwa hadi hatua za kudhibiti ajali mbaya zichukuliwe," TEPCO ilisema katika ripoti yake. Ripoti hiyo iliypowa jina la "Fundamental Policy Reform of TEPCO Nuclear Power Organisation" inasema mipango iliyofanywa kwa ajili ya maandalizi ya majanga ya asili ilikuwa haitoshelezi. Ilisema hatua za kinga dhidi ya ajali mbaya zilichukuliwa mwaka 2002 lakini hakuna kilichofanyika tangu wakati huo kwa kuhofia namna ambavyo hii ingeonekana kwa watu wanaoishi karibu na kiwanda hicho.
Imesema kuwa kulikuwepo na wasiwasi kwamba endapo hatua za kuzuia ajali mbaya zingechukuliwa, hili lingezua mashaka miongoni mwa jamii ya wakaazi wa eneo hilo, kwamba kuna matatizo na usalama wa mitambo ya kiwanda hicho. Iliongeza kuwa hatua yoyote ingeongeza kasi ya vuguvugu zinazopinga matumizi ya nyuklia. Kampuni hiyo ambayo ni moja ya makampuni makubwa zaidi duniani ya nishati ya umeme, ilikiri kuwa ilihofia uwezekano wa kushtakiwa endapo ingekiri kuwa usalama wa mitambo yake ulikuwa na walaakin.
Awali ilisema tsunami ilikuwa nje ya matarajio ya kisayansi
TEPCO ambayo imeshambuliwa kwa kuwa na usiri na kula njama na mamlaka yake ya udhibiti, ilitoa ripoti hiyo baada ya kuitisha paneli ya wataalamu wa nje kuangalia programu zake za nyuklia. Kukiri huko kwa kushindwa ni kinyume kabisaa na madai ya huko nyuma, kwamba tufani ya tsunami ilikuwa mbali zaidi ya matarajio ya kisayansi na kwamba hakuna namna yoyote wangeweza kujiandaa kukabiliana nayo.
Hata hivyo, paneli mbili tofauti zilizoundwa na serikali na bunge kuchunguza tukio hilo, ziligundua kuwa TEPCO ilikuwa imetahadharishwa kuhusiana na hatari zilizokikabili kiwanda hicho. Hatari hizo zilikuja kuwa kweli Machi 11, 2011 wakati tsunami iliposababisha tetemeko kubwa la ardhi lililokigaragaza kiwanda cha nyuklia cha Fukushima Daiichi, na kuharibu mifumo ya kupozea na hatimaye kuanza kuyeyuka kwa nishati katika mitambo hiyo.
Usafishaji kuchukua miongo kadhaa
Mitambo hiyo iliyoyeuka ilianza kusambaza miali ya rediolojia katika maeneo makubwa na kuathiri mashamba makubwa katika moja ya maeneo ya kuzalisha chakula nchini Japan. Hii iliwalaazimu pia maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao, na wengi wao bado wanaishi katika makaazi ya muda. Wengine wanaweza wasiruhusiwa kurudi kabisaa. Kusafisha kwa ardhi hiyo na kuvunjwa kwa mitambo hiyo kunaweza kuchukua miongo kadhaa wakati jamii nyingi zikitelekezwa.
Kampuni ya TEPCO ambayo tangu wakati huo imetaifishwa, inakabiliwa na madai ya mamilioni ya fidia, hii ikiwa juu ya gharama za kuvunja kiwanda cha Fukushima. Hakuna mtu aliyeripotiwa rasmi kufariki kutokana na ajali hiyo moja kwa moja, inagawa janga la asili linaaminika kuua karibu watu 19,000.
Mwandishi: Iddi Ismail/afpe
Mhariri: Sekione Kitojo