1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tetemeko la ardhi laua zaidi ya 1800 Nepal

26 Aprili 2015

Tetemeko kubwa la ardhi limeikumba Nepal Jumamosi na kuua mamia ya watu,kuangusha mnara wa karne ya 19 mjini Kathmandu pamoja na kusababisha maporomoko ya theluji milimani.

https://p.dw.com/p/1FEqJ
Juhudi za kuokowa manusura katika mji wa Kathmandu.(25.04.2015)
Juhudi za kuokowa manusura katika mji wa Kathmandu.(25.04.2015)Picha: Reuters/N. Chitrakar

Kuna repoti ya madhara makubwa katika maeneo ya nje ya kitovu cha tetemeko hilo lenye ukubwa wa kipimo cha Richter cha 7.9 maili 50 kutoka Pokhara mji wa pili kwa ukubwa nchini Nepal.

Tetetemeko hilo la ardhi ni kubwa kabisa kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 81 na pia limesababisha athari katika majimbo ya nchi jirani kaskazini mwa India na Bangladesh.

Wizara ya mambo ya ndani ya Nepal imesema watu zaidi ya 1800 wameshakufa na Idadi ya vifo inaweza kuongezeka sana na kwamba vifo vingi vimetokea katika Bonde la Kathmandu ambapo kuna wakaazi milioni 2.5 na viwango vya ubora wa majengo yake sio vizuri. Hakuna habari zilizoweza kupatikana mara moja kutoka maeneo ya nje katika nchi hiyo ya milima na helikopta zimekuwa zikijaribu kuangalia kutoka angani hali ya madhara

Naibu balozi wa Nepal mjini New Delhi Prasad Pandey amesema inahofiwa kuwa mamia ya watu wamekufa na kuna repoti ya kuwepo kwa uharibifu mkubwa kila mahala na kwamba sio tu katika baadhi ya maeneo ya Nepal bali nchi nzima imeathirika.

Majengo na mahekalu yageuzwa vifusi

Majengo kadhaa yameanguka katikati ya mji mkuu wa Kathmandu ya Kale yakiwemo mahekalu na minara iliojengwa karne nyingi zilizopita.

Watu wakiwa wamekusanyika kwenye Mnara Darahara mjini Kathmandu.(25.04.2015)
Watu wakiwa wamekusanyika kwenye Mnara Darahara mjini Kathmandu.(25.04.2015)Picha: P. Mathema/AFP/Getty Images

Miongoni mwao ni Mnara wa Dharahara wa ghorofa tisa ambao ni mnara wa kihistoria nchini Nepal uliojengwa na watawala wa kifalme katika miaka ya 1800 na kutambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu;Sayansi na Utamaduni UNESCO kama turathi ya dunia. Mnara huo umegeuzwa kifusi na inasemekana kwamba kuna watu kama hamsini walionasa chini ya vifusi.

Katika hospitali kuu mjini Kathmandu watu waliovunjika viungo na mikono wamekuwa wakikimbizwa kwenye hospitali hiyo.Watu wamejaa kwenye sebule za hospitali hiyo hadi viwanjani.

Picha za televisheni zimeonyesha watu wakipatiwa matibabu barabarani nje ya hospitali na maiti kadhaa zilizofunikwa mablanketi zikiwa zimepangwa mstari.

Kathmandu ni maskani ya mahekalu ya kale ya Wahindu. Picha zilizowekwa kwenye mitandao zinaonyesha vifusi vya majengo,barabara zikiwa na nyufa kubwa na wakaazi wakiwa wameketi barabarani na watoto wao wachanga.

Athari ni kubwa

Tetetemeko hilo pia limesababisha maporomoko ya theluji mlimani na kuzusha hofu kwa wapandaji milima waliokuwa katika Mlima Everest ambapo watu 10 wamekufa.

Hali baada ya tetemeko la ardhi Kathmandu. (25.04,.2015)
Hali baada ya tetemeko la ardhi Kathmandu. (25.04,.2015)Picha: Reuters/N. Chitrakar

Nepal ilikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi kuwahi kurekodiwa nchini humo hapo mwaka 1934 likiwa na kipimo cha 8.0 ambapo watu 8,500 walipoteza maisha yao.

Tetemeko la Jumamosi pia limetingisha miji ya kaskazini mwa India hadi mji ulioko mbali wa Lahore nchini Pakistan,Lhasa huko Tibet na Dhaka,Bangladesh.

Wakati kiwango hasa cha uharibifu na maafa bado hakijulikani kwa uhakika tetemeko hilo la ardhi yumkini likasababisha mzigo mkubwa kwa rasilmali za nchi hiyo ya kimaskini ambayo inajulikana zaidi kwa mlima wake mrefu kabisa duniani yaani Mlima Everest. Uchumi wa Nepal taifa lenye idadi ya watu milioni 27.8 unategemea sana utalii, hususan watu wanaokwenda nchini humo kwa ajili ya kutembea milimani na kukwea milima.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP

Mhariri : Bruce Amani