1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu kufuzu awamu ya mchujo Champions League

5 Novemba 2013

Mabingwa watetezi Bayern Munich na mabingwa mara tisa Real Madrid ni miongoni mwa timu nne zinazolenga kusajili ushindi wa nne mfululizo wa Champions League wiki hii ili kujikatia tikiti ya kucheza awamu ya mchujo

https://p.dw.com/p/1ABHH
Picha: picture-alliance/dpa

Paris St Germain na Atletico Madrid pia zimeshinda mechi zote tatu, huku Manchester City, ambao wameshinda mbili na kushindwa moja, wanaweza pia kujikatia nafasi ya awamu ya mchujo kama watawashinda CSKA Moscow katika kundi D.

Barcelona, ambao wameangusha pointi mbili, watafuzu kama watashinda nyumbani dhidi ya AC Milan katika kundi H nao Manchester United watapiga hatua kubwa ya kufikia awamu hiyo kama watawapiku Real Sociedad.

Bayern watakuwa ugenini dhidi ya Viktoria Plzen, wakati nao Paris St Germain wakicheza nyumbani na Anderlecht. Real Madrid wanaelekea kwa watani wao wa jadi Juventus huku nao Atletico Madrid wakiwakaribisha Austria Vienna. Shakhtar Donetsk watakuwa na kibarua dhidi ya Bayer Leverkusen, wakati nao FC Copenhagen wakiangushana na Galatasaray. Olympiakos watafunga kazi na Benfica.

Katika mechi nyingine za Jumatano Basel watapambana na Steaua Bucharest, Chelsea wawakaribishe Schalke 04, wakati nao Borussia Dortmund wakiwa wenyeji wa Arsenal. Napoli watakuwa wenyeji wa Olympique Marseille. Zenit St Petersburg watapimana nguvu na Porto nao Ajax Amsterdam wacheze na Celtic.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu