1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu zajikatia tiketi za robo fainali ya kombe la mataifa ya bara Afrika

27 Januari 2012

Wiki ya kwanza imekamilika katika kivumbi cha kombe la mataifa ya bara Afrika, kinachoendelea kule Gabon na Guinea ya Ikweta ambapo sasa ni harakati za kufuzu kwa mechi za robo fainali.

https://p.dw.com/p/13s6G
Wachezaji wa Angola washerekea bao lao dhidi ya Sudan
Wachezaji wa Angola washerehekea bao lao dhidi ya SudanPicha: dapd

Katika mechi za hii leo za kundi D kule Franceville nchini Gabon, kutakuwa na mchuano wa pili wa uhasimu wa afrika magharibi wakati Black Stars wa Ghana watakapokabana koo na Mali. Mali waliwanyamazisha Guinea bao moja kwa nunge katika mchuano wa kwanza wa vita vya afrika magharibi, na mchuano mwingine kama huo utakuwa wiki ijayo wakati Ghana watakapoumiza nyasi dhidi ya mahasimu wao Guinea.

Tathmini ya mchuano wa Ghana dhidi ya Mali

Black Stars wa Ghana kwa mara nyingine watatarajiwa kuwazaba Mali jinsi walivyofanya katika michuano yote ya nyumbani na ugenini katika mechi za kufuzu kwa kombe la dunia 2010. kocha wa Ghana Goran Stevanovic anakiri kuwa ni vigumu kwako ikiwa wewe ni mmojawapo wa timu zinazopigiwa upatu kabla ya kuanza kwa kivumbi hicho.

Naye kiungo wa kati wa Barcelona Seydou Keita ametwikwa jukumu kubwa kutokana na kutokuwepo kwa magwiji kama vile Mahamadou Diarra, Momo Sissoko na Fredrcik Kanoute ambao wamezitundika njumu zao katika soka ya kimataifa. Keita anasema Mali wana msukumo kuwashinda Ghana ambao wanaonekana kupigiwa upatu mno.

Tathmini ya mchuano wa Botswana dhidi ya Guinea

Katika mchuano mwingine wa kundi D hii leo Guinea na Botswana watakuwa na shinikizo la kushinda baada ya timu hizo mbili kushindwa katika mechi zao za ufunguzi. Ushindi kwa yeyote utaamusha matumaini yao, ambayo yalipatwa na pigo kubwa baada ya kushindwa michuano yao ya kwanza dhidi ya Mali na Ghana mtawalia.

Kocha wa Guinea Michel Dussuyert anasema wanafaa kupigana vikali ili kuwashinda Botswana ambao wana safu ngumu ya ulinzi. Alisema wataendelea kuimarika hasa ikizingatiwa ana kikosi cha chipukizi ambao wanahitaji ujuzi. Naye kocha wa Botswana Stanely Tshosane aliutaja mchuano huo wa Guinea kuwa ni sharti waushinde huku akitumia fursa hiyo kuomba marupurupu ya kifedha kupewa wachezaji wake. Alisema mchuano huo ndio utakaoamua hatima yao na hivyo ni muhimu na ni sharti waushinde.

Tshosane anasema wachezaji hao watajizatiti hata zaidi ikiwa watakuwa na hela kadhaa mifukoni mwao ikizingatiwa kuwa mapema mwezi huu walitishia kukataa kushiriki mchuano wa mwisho wa kupasha misuli moto dhidi ya Zimbabwe ili kushinikiza masharti yao ya kulipwa marupurupu yao baada ya kufuzu kwa fainali hizo.

Bayer Leverkusen yasema Michael Ballack hajaonyesha mchezo bora

Tukirejea hapa Ujerumani Bayer Leverkusen Michael Ballack ameshindwa kuonyesha mchezo bora katika miezi yake 20 ya kuwa katika klabu hiyo ya Bundesliga baada ya kujiunga nayo mwaka 2010 akitokea Chelsea. Afisa mkuu mtendaji wa klabu ya hiyo Wolfgang Holzhaeuser amesema nahodha huyo wa zamani wa Ujerumani aliyepoteza nafasi yake katika timu ya taifa, mwaka jana baada ya kukosa kushiriki fainali za kombe la dunia 2010 kwa sababu ya jeraha, hajaweza kutoa mchango wake kikamilifu kwa timu yake ya Leverkusen.

Mchezaji wa Bayer Leverkusen Michael Ballack
Mchezaji wa Bayer Leverkusen Michael BallackPicha: dapd

Leverkusen waliomaliza nambari mbili katika ligi ya ujerumani mwaka jana, hata hivyo wamefuzu kwa awamu ya 16 ya kombe la mabingwa ambako watakabana koo na Barcelona.

Bayern Munich yawaomba radhi mashabiki wake

Klabu ya Bayern Munich iliwadanganya mashabiki wake kwa kuwataka wajiunge na klabu hiyo katikaa ukursa wao wa tuvuti ya kijamii Facebook, baada ya kuwaahidi kuwa itamsajili mchezaji mpya nyota. Hivyo mashabiki wangeweza tu kumjua mchezaji huyo ikiwa wangejiunga na ukurasa wao wa facebook.

Hata hivyo baada ya wengi kufanya hivyo ili wamwone ni nani atakayesaidiana na Mario Gomez katika safu ya mashambilizi, walipokea ujumbe kuwa hakuna mchezaji yeyote aliyesajiliwa. Kwamba ilikuwa mbinu ya kuwafanya mashabiki wengi kujiunga na klabu hiyo. Mashabiki wengi walighadhabishwa na hatua hiyo: Lakini baadaye BAYERN iliomba radhi kuhusiana na tukio hilo la kuimarisha ushabiki wa klabu hhiyo na ambalo lilitibuka.

Taarifa kutoka kwa kwa klabu hiyo imesema haikuwa nia yao kuwakasirisha mashabiki kupitia mbinu hiyo mpya: awali klabu hiyo ilijitetea ikisema kila shabiki wa Bayern ni mchezaji wao mashuhuri wa 12. Hatua hiyo ya Bayern ilijiri baada ya timu ya taifa ya Ujerumani kutangaza mwezi jana kuwa imefikisha mashabiki milioni moja kwenye ukurasa wao wa Facebook. Ukurasa wa mashabiki wa timu hiyo unajaribu kushindana na timu ya taifa ya Uingereza.

Mwandishi: Bruce Amani

Mhariri: Mohammed Khelef