Trump aiomba mahakama kusitisha marufuku dhidi ya TikTok
28 Desemba 2024Rais mteule Donald Trump ameirai Mahakama Kuu ya Marekani kusitisha utekelezaji wa sheria inayoweza kuipiga marufuku programu maarufu ya mitandao ya kijamii, TikTok, au kulazimisha iuzwe, akisema anapaswa kupewa muda baada ya kuingia madarakani ili kutafuta "suluhisho la kisiasa" kwa suala hilo.
Mahakama inatarajiwa kusikiliza hoja za kesi hiyo tarehe 10 Januari.
Sheria hiyo inawataka wamiliki wa TikTok kutoka China, ByteDance, kuiuza kwa kampuni ya Marekani au kukabiliana na marufuku. Bunge la Marekani lilipiga kura mnamo Aprili kupiga marufuku mtandao wa TikTok au mmiliki wake, ByteDance ilaazimishwe kuiuza kabla ya tarehe 19 Januari.
TikTok, ambayo ina zaidi ya watumiaji milioni 170 nchini Marekani, na kampuni mama yake, wamepambana kuzuwia sheria hiyo. Hata hivyo, ikiwa mahakama haitatoa uamuzi upande wao na hakuna mchakato wa uuzaji utakaofanyika, programu hiyo inaweza kupigwa marufuku rasmi nchini Marekani mnamo tarehe 19 Januari, siku moja kabla ya Trump kuingia madarakani.
Msimamo huu wa Trump kuhusu TikTok ni kinyume na ule wa mwaka 2020, alipokuwa akijaribu kuizuia programu hiyo nchini Marekani na kulazimisha iuzwe kwa kampuni za Marekani kwa sababu ya uhusiano wake na China.
Hali hii pia inaonyesha juhudi kubwa za kampuni hiyo kujenga mahusiano mazuri na Trump na timu yake wakati wa kampeni za urais.
Soma pia: Trump apiga marufuku mahusiano na wamiliki wa Tik Tok
"Rais Trump hana msimamo wowote kuhusu madai ya msingi ya mgogoro huu," alisema D. John Sauer, wakili wa Trump ambaye pia ni chaguo lake la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Marekani.
"Badala yake, anaomba kwa heshima Mahakama itafakari kusimamisha tarehe ya mwisho ya uuzaji wa TikTok mnamo Januari 19, 2025, huku ikizingatia madai ya kesi hii, hivyo kuupa utawala unaokuja wa Trump nafasi ya kufanikisha suluhisho la kisiasa kwa maswali yaliyojadiliwa katika kesi hiyo," aliongeza.
Trump alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok, Shou Zi Chew, mnamo Desemba, saa chache baada ya rais mteule kueleza kuwa ana "nafasi ya upendeleo" kwa programu hiyo na kwamba anapendelea iendelee kufanya kazi Marekani kwa muda mfupi.
Rais mteule pia alisema alipokea mamilioni ya maoni kwenye jukwaa hilo la mitandao ya kijamii wakati wa kampeni zake za urais. TikTok haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni.
Kampuni hiyo hapo awali ilisema Wizara ya Sheria ya Marekani imepotosha kuhusu uhusiano wake na China, ikieleza kuwa injini yake ya mapendekezo ya maudhui na data za watumiaji zimehifadhiwa nchini Marekani kwenye seva za wingu zinazomilikiwa na Oracle Corp, huku maamuzi ya udhibiti wa maudhui yanayoathiri watumiaji wa Marekani yakifanywa nchini humo.
Soma pia: Meta, TikTok na X, wabanwa kuhusu usalama mtandaoni
Watetezi wa uhuru wa kujieleza waliiambia Mahakama Kuu siku ya Ijumaa kuwa sheria ya Marekani dhidi ya TikTok inafanana na mifumo ya udhibiti wa maudhui iliyowekwa na maadui wa kimabavu wa Marekani.
Wizara ya Sheria ya Marekani imeeleza kuwa udhibiti wa TikTok na China unaendelea kuwa tishio kwa usalama wa taifa, msimamo unaoungwa mkono na wabunge wengi wa Marekani.
Mwanasheria Mkuu wa Montana, Austin Knudsen, aliongoza muungano wa mawakili wakuu 22 siku ya Ijumaa kuwasilisha ombi kwa Mahakama Kuu kuidhinisha sheria ya kitaifa inayolazimisha uuzaji au marufuku ya TikTok.