Trump awasili Paris kufuatia mwaliko rasmi
13 Julai 2017Rais wa Marekani Donald Trump amewasili mjini Paris Ufaransa kwa ziara rasmi. Ziara hiyo inajiri siku ya sherehe ya kijeshi mjini Paris na Ikulu ya Marekani inatumai itampa Trump pumziko kidogo dhidi ya kashfa zinazomkabili nchini mwake.
Ndege iliyombeba rais Donald Trump Air Force One ilitua mjini Paris mapema leo, katika mwanzo wa ziara ya saa 24 ya Trump nchini Ufaransa kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais Emmanuel Macron. Ziara hiyo inaenda sanjari na siku ya kitaifa ya Ufaransa hapo kesho ya kuadhimisha miaka 100 ya ushiriki wa Marekani katika vita vikuu vya kwanza vya dunia ambayo huwa na gwaride la kila mwaka la siku ya Bastille.
Hii ikiwa mara ya kwanza kwa Trump kuzuru Ufaransa kama rais, inatarajiwa kuwa ziara hiyo itampa pumziko dhidi ya madai mazito yanayomzonga nchini mwake kuhusiana na tuhuma kuwa familia yake na wapambe wake walikuwa na mahusiano na Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.
Mswada wa kumuondoa Trump madarakani
Kando na hayo ni kuwa hapo jana, mjumbe wa chama cha Democrat wa California Brad Sherman, alikuwa mbunge wa kwanza kuwasilisha rasmi mswada wa kutaka Trump aondolewe madarakani.
Sherman ametaja visa vya uhalifu mkubwa na mdogo mdogo kuwa sababu za kutaka Trump aondolewe madarakani, akisema juhudi za Trump kuzuwia uchunguzi juu ya uhusiano wa Urusi na iliyokuwa timu ya kampeni yake, pamoja na uchunguzi dhidi ya msaidizi wake mkuu, zinamaanisha alikusudia kuhujumu uchunguzi na haki.
Hata hivyo juhudi hizo huenda zikaambulia patupu kutokana na wabunge wa chama cha Republican kuwa wengi zaidi bungeni. Msemaji wa White House Sarah Huckabee alipoulizwa na mwanahabari kuhusu kauli yake kuhusiana na mswada huo aliipuuzilia mbali kuwa mchezo wa siasa. "Ninafikiri ni kichekesho sana na mchezo wa kisiasa unaochusha ahsanteni sana."
Katika ziara ya Ufaransa, mazungumzo kati ya Trump na Macron yanatarajiwa kulenga juhudi za pamoja za kulikabili kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria. Trump na Macron , wanataka kuweka kando tofauti zao kuhusiana na biashara na mabadiliko ya tabia nchi na kupata msimamo wa pamoja watakapokutana leo, kujaribu kupata suluhisho la mzozo wa Syria pamoja na mikakati mipana zaidi katika kupambana na ugaidi.
Katika sherehe hizo muhimu za kuashiria wakati muhimu wa mageuzi ya Ufaransa, Trump atakuwa mgeni wa heshima, na pia atatembelea eneo alikozikwa aliyekuwa kiongozi wa kijeshi na kisiasa wa Ufaransa Napoleon. Trump baadaye atalakiwa kwa heshima ya kijeshi katika Hoteli des Invalides mjini Paris.
Wasiwasi wa viongozi dhidi ya Trump
Viongozi wa London, Berlin, Brussels, Paris na Ulaya wangali wanayo maswali kuhusu njia gani bora ya kushirikiana na Trump ambaye sera yake ya mfumo wa kuitenga Marekani imeathiri ushirikiano. Hata hivyo Macron anatumai kukuza uhusiano na Trump hali ambayo huenda ikamwezesha kushawishi sera za Marekani au kuepusha mikwaruzano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.
Ziara ya Trump Paris, ni ya pili katika bara la Ulaya mwezi huu na inakuja huku kukiwa na ufichuzi mpya juu ya kampeni yake ya kuwania urais.
Wakati huo huo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walifanya mazungumzo pamoja na mawaziri kutoka nchi hizo mbili leo katika ikulu ya Ufaransa mjini Paris.
Mwandishi: John Juma/DPAE/AFPE/
Mhariri: Iddi Ssessanga