1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kuwafukuza wahamiaji haramu

Isaac Gamba
14 Novemba 2016

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema anakusudia kuwafukuza wahamiaji  kati ya milioni 2 hadi milioni 3 wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria mara tu atakapokabidhiwa rasmi madaraka.

https://p.dw.com/p/2SeSK
USA Reince Priebus neuer Stabchef im Weißen Haus
Rais Mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/B. McDermid

Trump ameyasema hayo katika mahojiano yake ya kwanza kwa njia ya televisheni tangu alipotangazwa mshindi wa urais kufuatia  uchaguzi uliofanyika Jumanne iliyopita.  

 Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha CBS rais huyo mteule  ambaye sasa atakuwa  rais wa 45 wa Marekani amesema serikali yake itawaondoa nchini humo wahamiaji wenye rekodi ya uhalifu wakiwemo wanaojihusisha na madawa ya kulevya na kusisitiza kuwa wanaishi nchini humo kinyume cha sheria. Akisisitiza hilo alisema:

USA Donald Trump
Donald TrumpPicha: Getty Images/S. Olson

"Tunachotarajia kufanya ni kuwatafuta watu ambao ni wahalifu na wenye rekodi ya uhalifu, wanaojihusha na madawa ya kulevya, tunao wengi watu wa aina hii yawezekana wako kama milioni mbili na wanaweza kuwa hata milioni tatu, tutawafukuza nchini ama kuwaweka katika vituo maalum."

Akizungumzia juu ya ahadi yake aliyoitoa wakati wa kampeni ya kujenga ukuta kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico, Trump amesema ukuta alioahidi kujengwa unaweza usiwe ule uliojengwa kwa mawe au matofali lakini akasisitiza kuwa kutakua na uzio katika baadhi ya maeneo ya mpaka huo.

Udhibiti wa  mipaka 

Alisema iwapo kutakuwa na udhibiti mpakani basi hiyo itasaidia idara  inayohusika na masuala ya uhamiaji  pamoja na idara ya forodha nchini humo kuweza kufanya kazi yake barabara pamoja na kuwabaini wahamiaji wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.  wakati wa mikutano yake ya kampeni Trump aliahidi kujenga ukuta katika mpaka na Mexico na kusema gharama za ujenzi huo zitalipiwa na Mexico.  Hata hivyo serikali ya Mexico imesema haitalipa gharama hizo za ujenzi.

Wakati Trump akisisitiza kutekeleza baadhi ya ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni baadhi ya wahamiaji pamoja na makundi mengine yanayopinga kuchaguliwa kwake waliendelea kuandamana hapo jana wakipinga hatua yake ya kuwafukuza wahamiaji pamoja na hatua nyingine ambazo amepanga kuzichukua ambazo hawaziafiki. 

USA Präsidentschaftswahl Anti-Trump Proteste vor Trump Tower in New York
Maandamano katika mitaa ya mji wa New York katika jengo la Trump Tower Picha: picture-alliance/dpa/K. Hagen

Waandaaji wa maandamano hayo walibeba mabango yaliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza na kihispania yakisomeka " Chuki haitalifanya taifa hili kuwa kubwa " na kuwa wataendelea kuishi nchini humo.  Zaidi ya watu 1,000 walishiriki maandamano hayo yaliyoanza mchana na kuendelea hadi wakati wa jioni.

Trump ateua washauri wake

Wakati huohuo Donald Trump hapo jana (13.11.2016)ametangaza  kumteua mmoja wa wanasiasa waandamizi ndani ya chama cha Republican ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya taifa ya chama hicho  Reince Priebus kuwa mkuu wa utumishi katika Ikulu ya Marekani ambayo ni moja ya nafasi za juu kabisa katika serikali ya nchi hiyo huku pia akimteua aliyekuwa mwenyekiti wake wa kampeni Stephen Bannon kuwa mshauri wake mwandamizi.

USA Reince Priebus neuer Stabchef im Weißen Haus
Reince Priebus mshauri mwandamizi wa TrumpPicha: Reuters/M. Segar

Kwa upande mwingine Rais wa China Xi Jimping akizungumza hii leo  kwa njia ya simu na Rais mteule Donald Trump, wamekubaliana kukutana mapema ili kujadili uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu za kiuchumi duniani.  Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha serikali ya China CCTV.

Kabla ya uchaguzi, Trump alikuwa akiishambulia China akiita kuwa ni adui wa Marekani akiishutumu kushusha thamani ya pesa yake makusudi ili kuimarisha mauzo yake ya nje na kuahidi kusimama kidete dhidi ya nchi ambayo alidai inaiaona Marekani kama nchi ya kuburuzwa.

Mwandishi:  Isaac Gamba/DW/APE

Mhariri       :Gakuba Daniel