1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump: Sudan kuondolewa kwenye orodha ya wafadhili wa ugaidi

Yusra Buwayhid
20 Oktoba 2020

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Sudan itaondolewa kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili makundi ya kigaidi, ikiwa itakubali kutoa dola milioni 335 kuwalipa wahanga wa Kimarekani wa mashambulizi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/3k9z1
USA Donald Trump Wahlkampf in Arizona
Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture-alliance

Hatua hiyo itafungua milango kwa nchi hiyo ya Afrika kupata mikopo ya kimataifa na misaada inayohitajika kufufua uchumi wake uliporomoka pamoja na kuisaidia nchi hiyo kuwa ya kidemokrasia.

Akizungumza na kituo cha televisheni ya taifa, Waziri Mkuu Abdalla Hamdok ameliunga mkono tangazo hilo la Trump.

"Uamuzi huu utaisaidia Sudan kupata unafuu katika madeni yake. Leo hii tuna deni la zaidi ya dola bilioni 60. Uamuzi huu umetufungulia milango ya Sudan kuweza kupata afueni kutokana na deni hilo," amesema Hamdok.

Trump ametoa tamko hilo ikiwa zimebakia takriban wiki mbili hadi siku ya uchaguzi mkuu wa Marekani.

Afisa mmoja wa Marekani ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba makubaliano hayo pia yanaweza kuichochea Sudan kuboresha uhusiano wake wa kidiplomasia na Israel, kama zilivyofanya hivi karibu Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Uamuzi umepitwa na wakati

Marekani ilichukua uamuzi wa kuiweka Sudan katika orodha hiyo mnamo mwaka 1993, ikiamini rais wa wakati huo Omar al-Bashir alikuwa akifadhili makundi ya kigaidi.

sudanesischer Premierminister Abdalla Hamdok
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla HamdokPicha: picture-alliance/AA/M. Hjaj

Lakini wengi Sudan wanasema ni uamuzi uliopitwa na wakati, kwani Bashir aliondolewa madarakani mwaka jana, na taifa hilo limekuwa likitoa ushirikiano katika vita vya kupambana na ugaidi.

Kutokana na hali hiyo, inakuwa vigumu kwa serikali ya mpito ya Sudan kuweza kupata msamaha wa madeni unaohitajika haraka pamoja na ufadhili wa kigeni.

Kufuatia vuguvugu la maandamano ya mwaka jana yaliyomuondoa madarakani Bashir mnamo mwezi Aprili, Sudan hivi sasa inajaribu kuimarisha demokrasia lakini bado safari hiyo inayumba.

Serikali ya mpito ya kijeshi na raia hivi sasa ndiyo inayotawala nchi, huku kukiwa na matumainina ya kufanyika uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2022.

Hamdok amesema walianza mazungumzo na Marekani mwaka jana, ambayo yalituama zaiai kwenye suala la pesa. Na vyanzo vya kuaminika vimesema serikali ya Trump inaitaka Sudan iwalipe wahanga wa mashambulizi yaliyofanywa na mtandao wa al-Qaeda katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mnamo mwaka 1998.

Kiongozi wa mtandao wa al-Qaida Osama bin Laden, inaaminika alikuwa akiiishi nchini Sudan wakati wa mashambulizi hayo.

Vyanzo: (ap,rtre)