1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsangirai akutana na waziri wa serikali za wilaya wa Afrika Kusini

Charo, Josephat7 Aprili 2008

Lengo ni kutaka rais Mugabe ashinikizwe ajiuzulu

https://p.dw.com/p/Ddka
Kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) Morgan TsvangiraiPicha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, yumo nchini Afrika Kusini kutaka rais Robert Mugabe ashinikizwe ajiuzulu. Ziara yake nchini humo imefanyika wakati mahakama kuu ya Zimbabwe ikiahirisha uamuzi wake kuhusu ombi la upinzani kuitaka iilazimishe tume ya uchaguzi ya nchi hiyo itangaze matokeo ya uchaguzi wa rais, huku rais Robert Mugabe akichochea wasiwasi kabla kufanyika duru ya pili ya uchaguzi.

Chama cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change, MDC, kimesema kiongozi wake bwana Morgan Tsvangirai, yuko nchini Afrika Kusini hii leo kukutana na watu anaowaita kuwa muhimu huku akiitolea mwito jumuiya ya kimataifa imshinikize rais Robert Mugabe ang´atuke madarakani baada ya kutawala kwa miaka 28.

Msemaji wa chama cha MDC, Tendai Biti, amesema Tsvangirai alikwenda jana Afrika Kusini ambako anakutana na watu muhimu lakini hakutoa maelezo. Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, aliyejaribu kuongoza juhudi za kukipatinisha chama cha rais Mugabe cha ZANU-PF na chama cha upinzani cha MDC, amekwenda India kuhudhuria mkutano kati ya India na Afrika.

Msemaji mwingine wa chama cha MDC, Roy Bennet, amethibitisha kuwa Tsvangirai, akiwa katika ziara yake ya kwanza tangu uchaguzi wa rais kufanyika mnamo tarehe 29 mwezi uliopita, amefanya mikutano ya kibinafasi na anatarajiwa kurejea Zimbabwe baadaye leo.

Dola kuu ziingilie kati

Tsvangirai katika maoni yake yaliyochapishwa leo na gazeti la Uingereza, The Guardian, amezitaka dola kuu kama vile Afrika Kusini, Marekani na Uingereza zichukue hatua kuuondoa utawala wa mkono wa chuma wa rais Mugabe ulio wa maangamizi.

Wizara ya mashauri ya kigeni ya Afrika Kusini imesema haijui kuhusu shughuli rasmi za Tsvangirai alizopangiwa nchini humo. Msemaji wa wizara hiyo, Ronnie Mamoepa, amesema watu kutoka Zimbabwe wanaweza kwenda Afrika Kusini wakati wowote lakini hiyo haina maana wana shughuli rasmi za kufanya nchini humo. Inaripotiwa kwamba bwana Tsvangirai amepangiwa kusafiri kwenda katika taifa lengine lisilojulikana barani Afrika.

Mahakama yaahirisha uamuzi

Ziara ya Tsvangirai nchini Afrika Kusini imefanyika huku mahakama kuu ya Zimbabwe ikiahirisha uamuzi wake kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais. Huku uamuzi ukisubiriwa hapo kesho, jaji mkuu Tendai Uchena, amekanusha madai ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kwamba mahakama haziwezi kuisikiliza kesi hiyo.

Wakili wa upinzani, Alec Muchadehama, amesema jaji mkuu amekataa ombi la tume ya uchaguzi kwamba mahakama haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo. Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kutolewa hapo kesho mwendo wa saa nne asubuhi saa za Zimbabwe.

Chama tawala cha rais Mugabe cha ZANU-PF kinadai ushindi wa viti vya ubunge vinavyoweza kuubadili ushindi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC. Tayari vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kwamba chama cha ZANU-PF kinataka kura zote za uchaguzi wa rais zihesabiwe upya.

Mashamba ya wazungu yavamiwa

Wakati huo huo, wapiganaji wa zamani, wafuasi sugu wa rais Mugabe walioongoza operesheni ya kutumia nguvu kuyateka mashamba, wamejaribu kuingia katika baadhi ya mashamba ya wazungu yaliyosalia nchini Zimbabwe.

Chama cha wakulima wanaokuza mazao kwa ajili ya biashara, kinachowawakilisha wakulima wazungu waliosalia nchini humo, kimesema wafuasi wa rais Mugabe wameingia katika mashamba yasiyopungua 15 yanayomilikiwa na wazungu na kukikosoa chama tawala kwa kufanya kampeni ya ubaguzi wa rangi.

Rais Mugabe ambaye amekuwa akiitawala Zimbabwe tangu uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka wa 1980, anatafuta kuzusha machafuko ya kikabila na kuuharibia sifa upinzani kama chombo kinachotumiwa na nchi za magharibi kitakachobadili mageuzi yake kuhusu umilikaji wa ardhi.

Rais Mugabe amenukuliwa katika gazeti la serikali la The Herald lililochapishwa leo akisema na hapa namnukulu, "Ardhi lazima ibakie mikononi mwetu. Ardhi ni yetu na haipaswi hata kidogo kuingia mikononi mwa wazungu," mwisho wa kumnukulu.

Wakosoaji wanamlaumu rais Mugabe kwa mpango wa mageuzi ya sheria kuhusu umilikaji wa ardhi ulioharakishwa mnamo mwaka wa 2000, ambao umesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi nchini humo.

Waandishi waachiwa

Wakati haya yakiarifiwa, waandishi wawili wa habari raia wa kigeni wameachiwa huru kwa dhamana. Wandishi hao wametakiwa kulipa dola milioni 300 za Zimbabwe ikiwa ni sawa na dola 10,000 za Marekani.

Wakili wao, Harrison Nkomo, amesema muingereza huyo ameamriwa kuishi katika ubalozi wa Uingereza na mmarekani akaamriwa akae katika zahanati ya Dandaro kwa sababu alianguka na kupata majeraha mabaya alipokuwa akizuiliwa jela na hivyo anahitaji matibabu.

Barry Bearak mwenye umri wa miaka 58 na muingereza mwenye umri wa miaka 45, walikamatwa katika nyumba moja ya wageni mjini Harare Alhamisi wiki iliyopita na baadaye kushtakiwa kwa kuripoti kuhusu uchaguzi wa Zimbabwe bila vibali.

Wakili wa mmarekani mfanyakazi wa gazeti la New York Times na muingereza waliokuwa wakizuiliwa katika jela moja ya Zimbabwe alilalamika hii leo kuhusu usumbufu wakati wateja wake walipokuwa wakizuiliwa kwa siku ya tano.

Wakili Beatrice Mtetwa hapo awali aliwaambia waandishi wa habari mjini Harare kwamba jaji anayetakiwa kuisikiliza kesi ya wateja wake hayupo na jaji mkuu anayetakiwa kuamuru nani aishughulikie kesi hiyo pia hayupo.