Tume ya uchaguzi Congo yaahirisha kutoa matokeo
6 Januari 2019Matokeo ya awali, ambayo yalipangwa kutolewa leo Jumapili, sasa yatatolewa wiki ijayo, mkuu wa tume ya uchaguzi nchini humo CENI ameliambia shirika la habari la AFP masaa machache kabla ya muda wa mwisho kumalizika.
"Haitawezekana kutangaza matokeo siku ya Jumapili. Tunapinga hatua , lakini hatuna kila kitu bado," alisema Corneille Nangaa, bila ya kutangaza siku ya kutangaza matokeo hayo.
Baraza la maaskofu wa Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini Congo , CENCO, ambalo linawakilisha maaskofu wa Kikatoliki nchini humo , limeonya kwamba hasira za umma zinaweza kujitokeza iwapo matokeo ya mwisho hayatakuwa ya "kweli kwa mujibu wa matokeo halisi ya kura."
Kanisa linamjua mshindi
Kanisa katoliki lenye ushawishi nchini Congo, ambalo limetoa zaidi ya wachunguzi wa uchaguzi 40,000 , lilisema siku ya Alhamis kwamba linamjua mshindi wa uchaguzi huo , lakini halikumtaja.
Katika barua kwa Nangaa siku ya Jumamosi, rais wa baraza hilo la CENCO Marcel Utembi amesema kwamba , kutokana na uchelewesho huo, "Iwapo kutakuwa na vuguvugu la maandamano ya umma itakuwa ni jukumu la CENI."
Uchaguzi huo wa Desemba 30 ulishuhudia wagombea 21 wakipambana kuwania kuchukua nafasi ya rais Joseph Kabila , ambaye ameitawala nchi hiyo kubwa , iliyokumbwa na mizozo kwa karibu miaka 18.
Miongoni mwa wale walioko katika nafasi za mbele ni pamoja na mrithi aliyeteuliwa na Kabila Emmanuel Ramazani Shadary na wagombea wawili wa upinzani, mwanasiasa wa siku nyingi mwenye ushawishi mkubwa Felix Tshisekedi na Martin Fayulu ambaye amejitokeza hivi karibuni.
DRCongo haijabadilisha kiongozi kwa amani
Anayetafutwa ni mwanasiasa kiongozi katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini ambayo haijawahi kuwa na kipindi cha madadiliko ya amani ya utawala tangu nchi hiyo kujipatia uhuru kutoka Ubelgiji mwaka 1960.
Kabila alikuwa aondoke madarakani miaka miwili iliyopita, lakini aling'ang'ania madarakani, na kuzusha maandamano ya umma ambayo yalikandamizwa kikatili, na kuuwa watu kadhaa.
Uchaguzi, ambao ulitanguliwa na kucheleweshwa mara kwa mara, ulifanyika katika hali ya utulivu. Lakini hali ya wasi wasi imejijenga katika muda wa kipindi cha mchakato wa kuhesabu kura, huku kukiwa na hofu kwamba matokeo yanaweza kuchakachuliwa ili kumuweka Shadary madarakani ambaye anaungwa mkono na Kabila.
Tume ya uchaguzi iliahidi kutangaza matokeo ya awali Jumapili (06.01.2019), na kufuatiwa na tangazo rasmi la matokeo ya uchaguzi hapo Januari 15.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Jacob Safari Bomani