1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Twitter kuimarisha usalama wa akaunti nchini Marekani

18 Septemba 2020

Twitter imesema inaimarisha usalama wa akaunti za watu mashuhuri kama njia ya kinga kabla ya uchaguzi wa Novemba 3 nchini Marekani huku jaji wa mahakama moja nchini humo akizuia mabadiliko ya huduma za posta yenye utata

https://p.dw.com/p/3ifh7
Symbolbild Twitter Account von Donald Trump
Picha: picture-alliance/Geisler-Fotopress

Mtandao wa twitter utatumia mifumo bora zaidi ya kutambua shughuli zozote zinazozua mashaka na kuimarisha ulinzi unaokusudiwa kuzuia udukuzi wa akaunti. Katika chapisho la blogi, kundi la usalama la kampuni hiyo ya kiteknologia limesema kuwa kutekeleza mikakati hiyo ya kiusalama ni hatua muhimu ya kinga. Mtandao wa twitter umesisitiza kuwa unalenga kuziweka akaunti hizo za watu mashuhuri salama wakati wa uchaguzi huo na kwamba akaunti hizo zitahitaji nywila thabiti. Twitter pia imesema kuwa itawezesha mfumo utakaohitaji uthibitisho kupitia barua pepe ama nambari ya simu.

Wakati huo huo Jaji Stanley Bastian wa mji wa Yakima katika mji mkuu Washington, amesema kuwa anatoa maagizo ya zuio la kwanza la kitaifa liliombwa na majimbo 14 yalioishitaki serikali ya Trump na huduma ya posta ya nchi hiyo. Majimbo hayo yalipinga sera ya huduma ya posta inayojulikana kama'' wacha nyuma'' ambapo malori yamekuwa yakiondoka katika vituo vya posta kwa wakati bila ya kujali iwapo kuna barua nyingine za kuchukuliwa. Pia walitaka huduma hizo za posta kuzipa kipaumbele  barua za uchaguzi.

USA Präsidentschaftswahlen 2020 | Joe Biden in Pittsburgh
Joe Biden- Mgombea urais wa chama cha DemocraticPicha: Reuters/A. Freed

Huku hayo yakijiri, mgombea urais wa chama cha Democratic nchini humo Joe Biden amesema Urusi itachukuliwa hatua kwa kuingilia uchaguzi wa Marekani iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi wa urais wa Novemba 3. Wakati wa mahojiano na shirika la habari la CNN jimboni Pennsylvania hapo jana, Biden aliulizwa kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu tamko hilo lakini akakataa kusema kile alichokimaanisha. Lakini wakati Biden akiitaja Urusi kuwa kitisho kwa uchaguzi, Rais Trump kwa upande wake anazungumzia kitisho tofauti. Trump anasema kuwa tishio kubwa ni magavana kutoka vyama vya upinzani kudhibiti kura, mamilioni ya kura. na kwamba kwake yeye hilo ni tishio kubwa zaidi kuliko nchi za nje, kwa sababu mambo mengi yaliosemwa kuhusiana na mataifa ya nje yalibainika kutokuwa ya kweli.

Mashirika ya ujasusi ya Marekani yanaamini kuwa Urusi inatumia mikakati mbali mbali kumdhalilisha Biden kabla ya uchaguzi huo wa Novemba na kwamba watu wanaoshirikiana na ikulu ya rais ya Urusi, Kremlin wanaimarisha juhudi za kuchaguliwa tena kwa rais Donald Trump. Urusi pia iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016 kumsaidia Trump kumshinda mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton.