Ubunifu wa Afrika katika vita dhidi ya Corona
Shirika la afya duniani WHO limeisifu Afrika kwa ubunifu ambao bara hilo linautumia kupambana dhidi ya virusi vya corona. Hii ni baadhi ya mifano ya ugunduzi unaoweza kuokoa maisha.
Mashine ya kupumua ya kujitengenezea
Mjini Nairobi, Kenya, wananfunzi wa udaktari wanafanya majaribio ya mashine ya kupumua inayoendeshwa kwa computer katika kituo cha biashara na ubunifu cha chuo kikuu cha Kenyatta. Watafiti kote Afrika wanatafuta njia za kutengeneza mashine zao za kupumua, vifaa vya kujikinga na vitakatishi vya mikono, kwa sababu mataifa kama Marekani yamenunua akiba yote duniani.
Suluhisho rahisi
Pia Vincent Ssembatya, Profesa wa chuo kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda ametengeneza mashine za kupumulia za gharama nafuu, kusaidia mfumo dhaifu wa afya nchini humo. Ameshirikiana na kampuni ya magari ya Kiira Motors. "Kila moja anataka bidhaa hiyo hiyo, hivyo Afrika ina fursa ndogo sana ya kuzipata," alisema Ssembatya katika mazungumzo na DW.
Kituo cha ubunifu Senegal
Wanafunzi wa uhandisi nchini Senegal wamejiunga na mapambano ya nchi yao dhidi ya janga la corona: Gianna Andjembe, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika masuala ya umeme, anaonesha moja ya mashine ya kisasa ya kutakatisha alioitengeneza mwenyewe. Wanafunzi hao wanataka kutumia ujuzi wao wa kitaaluma kuzipunguzia shinikizo wodi za hospitali.
Dk. Car achukua jukumu la kuwasiliana na wagonjwa
Roboti hii ndogo kwa jina Dk. Car ni ugunduzi wa wanafunzi wa Senegal pia. Kazi yake ni kupima shinikizo la damu na kiwango cha joto kwa wagonjwa wa corona. Madaktari wanamdhibiti Dk. Car kupitia kamera aliyofungiwa na app, na hivyo kuwasiliana na wagonjwa bila kujiweka wenyewe hatarini. Watu walioko maeneo ya vijijini yasiofikiwa kwa urahisi wanaweza kufikiwa pia kwa njia hii.
Hata umeme unapokatika
Nchini Ethiopia, mgunduzi kijana, Ezedine amebuni miongoni mwa mambo mengine, mashine ya kupumulia na kifaa cha utakatishaji mikono bila kugusa. Tayari ugunduzi wake 13 kati ya 20 umepata hatimiliki. Mashine yake ya kielektroniki ya kutoa sabuni imejengewa sensa ndani, ambayo inaweza kuendeshwa kwa pedeli wakati umeme unapokatika.
Michoro ya rangi katika mfumo wa 2D
Hakuna mipaka kwa ubunifu barani Afrika. Kuanzia Lagos hadi Nairobi, wasanii hutumia kuta za nyumba za miji yao kutukumbusha juu ya kanuni za kujilinda: Kuweka umbali kati ya mtu na mtu, Kuosha mikono, na kuvaa barakoa wakati wote. Kazi hii ya sanaa inakutikana katika eneo la mabanda la Kibera mjini Nairobi.
Mtindo wa nywele wa Corona
Kwa misuko hii watu wenyewe wamegeuka onyo: "Kwa mtindo wa corona tunataka kuwaomba watu waweke umbali kati yao, wavae barakoa na waoshe mikono yao mara kwa mara kwa vitakatishaji, ili kujilinda," alisema mgunduzi Mable Etambo kutoka Kibera. Pia anatumia rangi za kirusi cha corona kufikisha ujumbe wake.
Chakula cha lishe mlangoni
Hatua za kitaifa za kuzuwia kusambaa kwa covid-19 zimefanya iwe vigumu kwa watu kutafuta chakula. Kampuni moja ya teknolojia nchini Zimbabwe, Fresh In A Box, inawasilisha vyakula kutoka mashambani kwa wakulima hadi mlangoni. Kampuni hiyo inatumia app, bajaji za magurudumu matatu kusambaza vyakula: Chakula cha lishe huku ukiepuka mgusano. Na kwa anaetaka, anaweza kuagizia pia barakoa.
Uhamishaji wa maarifa katika karantini
Kufungwa kwa shule kote Afrika kumefanya uhudhuriaji darasani kuwa mgumu. Suluhisho lilihitajika. Nchini Tanzania kwa mfano, wanafunzi wanaweza kujifunza kwa uhuru kupitia jukwaa la mtandaoni la "Smartclass". Jukwa hilo humuunganisha mwanafunzi na waalimu 5000, ili vijana waendelea kusoma licha ya karantini.
Ufuatiliaji wa janga
Mitandao ya kijamii na apps vinageuka silaha dhidi ya corono kila mahala. Nchini Nigeria na Ghana, app ya Covid-19 Traige Tool inawawezesha watumiaji kutathmini hatari yao ya kuambukizwa virusi vya corona. Serikali ya Afrika Kusini inatumia Whatsapp kujibu maswali kuhusu covid-19. Na wanafunzi wa zamani mjini Cape Town wametengeza app ya kuzuwia kuenea kwa habari za uongo.