1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Halmashauri ya AU: Dlamini-Zuma amtia kiwewe Jean Ping

Admin.WagnerD12 Julai 2012

Mwanadiplomasia kutoka Gabon, Jean Ping anapigana kufa kupona kunusuru wadhifa wake kama mkuu wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika. Mshindani wake ni Nkosazana Dlamini-Zuma kutoka Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/15W6l
Jean Ping, Mkuu wa halmashauri ya Afrika aliyemaliza muhula wake wa kwanza.
Jean Ping, Mkuu wa halmashauri ya Afrika aliyemaliza muhula wake wa kwanza.Picha: Reuters

Kwa kawaida, Ping mwenye umri wa miaka 69, na aliyeiongoza halmashauri hiyo tangu mwaka 2008, angechukulia kuchaguliwa kwake kwa mara ya pili kama jambo la kawaida - kwa kuzingatia sheria ya Umoja wa Afrika inayompa fursa mwenyekiti anayemaliza muda wake kuongoza muhula wa pili. Lakini ushindani unaoonyeshwa na Dlamin-Zuma umemtia kiwewe Ping na kumkosesha amani.

Mwanzoni mwa wiki hii, Ping aliripuka na kulaumu kile alichokiita kampeni chafu inayoendeshwa na Afrika Kusini, kuharibu jina lake alilolijenga kwa muda mrefu, na kuvuruga kampeni zake. Nakataa kushusha hadhi ya kampeni hizi na natumai na wengine wanaoshiriki uchaguzi huu wataendesha kampeni safi zinazoleta heshima kwa bara letu, alisema Ping.

Nkosazana Dlamini Zuma.
Nkosazana Dlamini Zuma.Picha: AP

Jaribio la pili la kutafuta mshindi
Baada ya wagombea hao wawili  kushindwa kupata theluthi mbili ya kura zinazotakiwa katika mkutano wa Januari mwaka huu, watakabiliana tena Julai 15 mjini Addis Ababa Ethiopia, ambapo maamuzi ya nani kashinda yatatolewa siku inayofuata. Lakini jambo linalojitokeza katika uchaguzi huu ni mgawanyiko wa mataifa yanayozungumza Kifaransa na yale yanayozungumza Kiingereza.

Dlamini-Zuma anaungwa mkono na mataifa mengi ya kanda inayozungumza Kiingereza kusini mwa Afrika, ambayo haijwahi kuongoza Halmashauri kuu ya Afrika tangu kuanzishwa kwake muongo mmoja uliyopita. Wanaomfahamu mwanamama huyo wanasema anaichukulia kazi yake kwa uzito mkubwa na ni mtawala mzuri.

Lakini wakosoaji wake wanasema sura yake ya ukali inamuweka mbali na watu, ingawa wote wanakiri kuwa ni mchapa kazi na mwenye uwezo wa kipekee. Kama atachaguliwa siku ya Jumapili, atakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza  halmashauri kuu ya  Umoja wa Afrika.

Nkosazana Dlamini-Zuma ni nani?
Nkosazana Dlamini-Zuma alizaliwa tarehe 27 Januari 1949, katika mkoa wa mashariki wa KwaZulu-Natal na alianza kushiriki shughuli za kisiasa akiwa shuleni. Katika miaka ya 70 alienda uhamishoni na alisoma katika vyuo vikuu vya Bristol na Liverpool nchini Uingereza, huku akisaidia kuandaa vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi nje ya nchi yake. Aliolewa na rais Jackob Zuma mwaka 1982 na kuwa mke wake wa tatu, kabla ya kuachana naye mwaka 1998.

Mkutano wa Umoja wa Afrika ukiendelea mjini Addis Ababa.
Mkutano wa Umoja wa Afrika ukiendelea mjini Addis Ababa.Picha: dapd

Anakumbukwa kwa kuanzisha sheria iliyoufanyia marekebisho mfumo wa afya nchini Afrika Kusini, na kuwawezesha maskini kupatiwa huduma za afya bure, lakini pia alikosolewa kwa kuipigia chapuo dawa ya ukwimwi ambayo ilikuja kuthibitika kuwa haifanyi kazi. Uzoefu wake kama Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini, unamuweka katika nafasi nzuri ya kuongoza tume ya Afrika.

Kwa upande wa pili, mpinzani wake Jean Ping, licha ya kukosolewa kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti wakati wa migogoro nchini Libya na Cote d'Ivoire, wanamsifu kwa kuiunganisha Afrika na wadau muhimu kama vile Uturuki, India na muhimu zaidi China, ambayo ilidhamini ujenzi wa makao makuu  mapya ya Umoja wa Afrika kwa kitita cha dola za marekani milioni 200 na kukabidhi jengo hilo mwaka jana.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.