Uchaguzi mkuu wafanyika leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
28 Novemba 2011Matangazo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inafanya uchaguzi mkuu hii leo. Uchaguzi huo unafanyika licha ya kuwepo hofu kuwa ungecheleweshwa kutokana na matatizo ya utaratibu na usafirishaji wa vifaa vya kupigia kura. Miito ilitolewa na wakosoaji kutaka uchaguzi huo uchunguzwe upya kutokana na kasoro zilizojitokeza. Rais wa sasa, Joseph Kabila, anashindana na wagombea wengine 10 kuwania wadhifa wa urais, huku wagombea 18,500 wakishindania viti 500 vya ubunge. Mkuu wa tume huru ya uchaguzi nchini humo, Daniel Ngoy Mulunda, alisema jana kwamba nchi hiyo itaandaa uchaguzi wa amani na halali na kudhihirisha kwamba wakosoaji wa mchakato mzima wa uchaguzi huo walikosea katika kutoa tathmini yao.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef