Uchaguzi wa Afrika Kusini.
22 Aprili 2009Wafuasi wa ANC walijitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi uliofanyika leo. Kinara wa ANC Jacob Zuma alipiga kura yake nyumbani kwake huko KwaZulu Natal, huku kigogo wa siasa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela akipiga kura yake mjini JohannesBurg.
Wafuasi wa chama tawala cha African National Congress- ANC walimpokea kwa shangwe kinara wa chama hicho, Jabob Zuma, alipofika kupiga kura yake huko KwaZulu Natal.
Miaka 15 tangu kuingia madarakani, chama tawala cha ANC kinapigania kudhibiti wingi wake wa viti bungeni- upinzani huu unatoka kutoka chama cha COPE, chama kipya kilichoundwa baada ya mgawanyiko ndani ya ANC.
Tume ya uchaguzi imebashiri idadi kubwa ya watu wamejitokeza kupiga kura, na kufanya uchaguzi huu kuwa mkubwa kabisa katika historia ya Afrika kusini. Watu milioni 23 wamejiandikisha kupiga kura kuwateua wawakilishi wa viti 400 vya bunge la nchi hiyo.
Licha ya kibaridi kikali cha asubuhi, foleni ndefu zilionekana katika vituo vya kupigia kura....na wengi walikuwa na matarajio mengi waliposubiri katika foleni kushirika katika zoezi hili la demokrasia -walisema wanatumai watakaoteuliwa wataimarisha hali ya maisha ya raia nchini Afrika Kusini.
Kigogo wa siasa za Afrika Kusini Nelson Mandela- akiwa amevalia mavazi yenye rangi ya chama cha ANC alipokewa kwa shangwe alipowasili kupiga kura yake mjini Johannesburg.
Taratibu zote za uchaguzi zilikwenda kama zilivyopangwa, hakukuwa na matatizo yeyote, ila maeneo kadhaa tu ndiyo yaliyoripoti kucheleweshwa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura. Jumla ya wachunguzi 300 wa kimataifa wapo nchini Afrika Kusini kuchunguza shughuli hii nzima ya uchaguzi inavyoendeshwa.
Dkt. Salim Ahmed Salim anayeongoza ujumbe wa Umoja wa Afrika kusimamia uchaguzi huo Afrika Kusini anasema shughuli nzima ilikuwa tulivu na yenye nidhamu.
Mshindi wa tuzo la amani la Nobel, Askofu mkuu Desmond Tutu alisema msisimko katika uchaguzi huu ni wa kutia moyo- kuwa chama cha ANC pia kinapata upinzani, Tutu alisema hii ni ishara ya kukomaaa kwa demokrasia.
Matokeo kamili uchaguzi huu yanatarajiwa mwishoni mwa wiki. Chama cha ANC hata hivyo kinapata upinzani kutoka chama cha COPE kilichoundwa na wanachama waliojitoa ANC na wanaomuunga mkono rais wa zamani Thabo Mbeki.
Chama rasmi cha upinzani cha Demokratic Alliance pia kinatarajiwa kupata viti kadhaa, ingawa wachanganuzi wa kisiasa wanasema hakitopata kuungwa mkono sana, kwa sababu ni chama wengi weusi wa Afrika Kusini wanakilinganisha na chama cha watu weupe walio wachache Afrika Kusini.
Mwandishi: Munira Muhammad/ AFP, REUTERS
Mhariri: Abdulrahman.