UEFA: Atletico na Leipzig kucheza kama kawaida
10 Agosti 2020Matangazo
Shirikisho la vyama vya kandanda Ulaya – UEFA limesema mechi ya robo fainali kati ya Atletico Madrid na RB Leipzig itaendelea kama ilivyopangwa Alhamis licha ya watu wawili wa klabu hiyo kupatikana na virusi vya corona.
Klabu hiyo haikusema kama watu hao wawili ni wachezaji, wakufunzi au maafisa. Lakini vyombo vya habari Uhispania vinasema ni wachezaji. Atletico imesema raundi nyingine ya vipimo imefanywa leo. Watu hao wawili wamejiweka katika karantini majumbani mwao.
Klabu hiyo imefuta mazoezi yao ya mwisho leo kabla ya kwenda Lisbon. Msemaji amesema wanasubiri kwanza vipimo vya leo.
Mechi za robo fainali zitaanza Jumatano mjini Lisbon, wakati Atalanta ya Italia itakutana na Paris Saint-Germain na fainali itakuwa Agosti 23.