1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Mpox wazidi kuenea Burundi

18 Desemba 2024

Ugonjwa wa Mpox unaendelea kuripotiwa Burundi, waathiriwa zaidi wakitajwa kuwa vijana.

https://p.dw.com/p/4oJk0
Mgonjwa wa Mpox akipata matibabu
Mgonjwa wa Mpox akipata matibabu Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mkurugenzi wa kituo cha kukabiliana na magonjwa yanayoambukia Daktari Nyandwi Joseph anasema kamati ya kukabiliana na Mpox tayari imechapisha kitabu kinakachoonesha dalili za ungonjwa huo, kinga, na matibabu yake.

Kitabu hicho kitaenezwa hivi karibuni katika hospitali, zahanati na shule pamoja na sehemu nyingine za umma Burundi.

Tangu kuripotiwa mripuko wa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya nyani mwezi Septemba mwaka huu, Burundi imeorodhesha watu zaidi ya 1874 walioambukiwa. Kati ya hao, asilimia 56 wakitajwa kuwa wanaume na asilimia 44 wakiwa ni wanawake, huku asilimia 60 ya walioambukiwa wakitajwa kuwa vijana.

Juhudi za kukabiliana na Mpox

Daktari Joseph Nyandwi anayeongoza kamati ya kukabiliana na ugonjwa huo, anasema bado Mpox ipo Burundi, licha ya kuwa kasi ya maambukizi inaonekana kupungua.

Chanjo za Mpox zikisafirishwa
Chanjo za Mpox zikisafirishwaPicha: Justin Makangara/REUTERS

Ili kukabiliana na ugonjwa huo juhudi mbali mbali zimekuwa zikiendeshwa, na kwamba timu ya wataalam imechapisha kitabu kinachoorodhesha  dalili za ugonjwa huo, jinsi ya kinga, na matibabu ya ugonjwa huo.

Daktari Joseph Nyandwi anasema kitabu hicho kitasaidia mno katika kukabiliana na janga hilo la Mpox

"Nchi inakabiliwa na janga la Mpox, wataalam hao wamekusudia kutangaza uwepo wa ugonjwa huo, dalili zake, vipimo , na matibabu pamoja na kinga dhidi ya ugonjwa huo. Hii ni hatua muhimu kwani itapewa wote wanao husika na kuwafuatilia walokutikana na virusi vya Mpox," alisema Dokta Nyandwi.

Vijana wengi waambukizwa

Kwa upande wake Daktari Liliane Nkengurutse afisa kwenye wizara ya afya anayehusika na kukabiliana na magonjwa anasema juhudi zinaelekezwa zaidi kwa wakurugenzi wa shule na walimu, kwani imedhihirika kuwa ugonjwa huo unawapata zaidi vijana.

Utengenezaji wa chanjo za Mpox
Utengenezaji wa chanjo za MpoxPicha: abaca/picture alliance

"Asilimia 60 ya waloambukizwa na ugonjwa huo ni vijana na wengi ni katika mji mkuu Bujumbura. Hivyo tumekuwa tukiwahamasisha wakurugenzi wa shule na waalim kujuwa dalili za ugonjwa huo, ili atakate onekana na dalili asiweze kuwaambukiza wengine," alisema Dokta Nkengurutse.

Hata hivyo katika mitaa mbali mbali ya mji mkuu Bujumbura hususan katika maeneo ya umma, umakini na hata ufahamu juu ya Mpox hauzingatiwi.

Maeneo mengi ya umma kama mbele ya milango ya soko, shule na kwingineko kumetengwa ndoo za maji na sabuni ila haizitumiwi ipasavyo.