1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Italia kuzuia uingizaji silaha Libya

15 Juni 2016

Ujerumani na Italia zinasema ziko tayari kuunga mkono juhudi mpya za kuzuwia kuingizwa silaha kinyume na sheria nchini Libya - siku moja baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudi hizo.

https://p.dw.com/p/1J71n
Meli iliyosheheni wakimbizi katika bahari ya Mediterenia Karibu na fukwe za LibyaPicha: Reuters/EUNAVFOR MED

Walikuwa mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili,Ursula von der Leyen wa Ujerumani na Roberta Pinotti wa Italy waliotangaza uamuzi huo leo hii. Uamuzi wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa utaziruhusu manuari za Umoja wa ulaya kuanzisha opereshini zake katika bahari ya Mediterenia,zilizopewa jina-Sofia,opereshini zitakazosaidia kuimarisha marufuku ya silaha kwa Libya. Watu wameingiwa na hofu kwamba wanamgambo wa dola la Kiislamu nchini Libya wanapatiwa silaha kupitia bahari ya Mediterenia.

Umoja wa Ulaya umeamua kuanzisha opereshini Sophia tangu mwaka jana ili kupiga doria katika mwambao wa Libya na kuwakamata watuhumiwa wanaowaingiza wageni kinyume na sheria. Zaidi ya kusimamia juhudi za kuimarisha marufuku ya silaha,

Umoja wa Ulaya utapendelea pia kuona operesheni Sophia ikihusika na kuwapatia mafunzo walinzi wa fukwe nchini Libya.

Ujerumani na Italy zinasubiri mwongozo wa Umoja wa Ulaya

Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya bibi Federica Mogherini anatarajiwa kuratibu mwongozo wa opersheni hiyo."Tutasubiri mwongozo huo,na baadae tutatathmini vipi Ujerumani inaweza kuchangia" amesema waziri wa ulinzi wa Ujerumani bibi Ursula von der Leyen mbele ya waandishi habari,pembezoni mwa mkutano wa jumuia ya kujihami ya NATO mjini Brussels.

Genf EU-Außenbeauftragte Federica Mogherini zu Syrien-Krieg
Mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya Federica MogheriniPicha: picture-alliance/Zuma Press/X. Jinquan

"Kuna utayarifu mkubwa miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya wa kutaka kusaidia" amesema hayo waziri wa ulinzi wa Italy Roberta Pinotti aliyeongeza tunanukuu:"Na sisi pia tuko tayari".

Libya inazongwa na mzozo wa kisiasa tangu mtawala wa zamani Muammar Gaddafi alipong'olewa madarakani mwaka 2011.Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa,kuna zisizopungua milioni 20 nchini Libya nchi yenye wakaazi milioni sita.

Vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa vinasonga mbele Sirte

"Nchi kama Libya inayojikuta katika hali tete haiwezi kuachiwa kusheheni silaha kama hivi,"amesema waziri wa ulinzi wa Ujerumani bibi Ursula von der Leyen.

Deutschland Airbus A400M Militärtransporter der Luftwaffe ILA Ursula von der Leyen
Waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Wakati huo huo vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa vimesema vimejiimarisha katika ncha ya kaskazini ya mji wa Sirte,na wamewatimua washambuliaji wa IS wakiwa katika opereshini ya kuiteka ngome hiyo ya wanamgambo wa itikadi kali Afrika kaskazini.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga