1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaemewa na wakimbizi

13 Septemba 2015

Mamlaka za kiserikali nchini Ujerumani zimeonya Jumapili (13.09.2015) kwamba wafanyakazi wao na wale wa kujitolea wameemewa kupindukia katika juhudi zao za kuwakaribisha wahamiaji wanaofikia 450,000 hadi sasa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1GVrm
Wahamiaji wakiwa wamelala katika kituo kikuu cha reli mjini Munich.
Wahamiaji wakiwa wamelala katika kituo kikuu cha reli mjini Munich.Picha: Reuters/Michaela Rehle

Mpango wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya kuwagawa waomba hifadhi katika nchi za Umoja wa Ulaya yumkini ukapelekea mjadala mkali wakati wa mazunguzo ya mawaziri wa mambo ya ndani hapo Jumatatu mjini Brussels ambapo nchi za Ulaya mashariki wanachama wa umoja huo zinatarajiwa kukabiliwa na shinikizo jipya la kukubali utaratibu wa kugawana wahamiaji hao kwa mafungu.

Munich kituo kikuu cha reli kuingia Ujerumani kutokea Hungary kwa kupitia Austria Jumapili kimewapokea wahamiaji wapya 3,000 baada ya kupokea wengine 13,000 Jumamosi usiku.

Kwa mujibu wa kiongozi wa utawala wa Jimbo la Bavaria ya Juu Christoph Hillenbrand shirika la reli la Ujerumani imebidi liwapeleke wakimbizi Berlin kwa kutumia treni ya kasi ya safari ya kawaida na kuwatafutia nafasi wateja wao katika safari nyengine za treni.

Munich ukingoni kusambaratika

Jarida la Ujerumani la kila Jumapili Bild am Sonntag katika makala yake ilioipa kichwa cha habari "Munich ukingoni kusambaratika " imemkariri Hillenbrand akisema hafahamu tena namna ya kukabiliana na wimbi hilo la wahamiaji.Hapo Ijumaa meya wa Munich Dieter Reiter ametowa wito kwa majimbo 16 ya Ujerumani kujiunga nayo kutowa msaada.

Wahamiaji wanaowasili Munich.
Wahamiaji wanaowasili Munich.Picha: imago/M. Westermann

Wakimbizi 500 wameondoka Munich Jumapili asubuhi kwa kutumia treni maalum kuelekea Dortmund mji wa jimbo la North -Rihine Wastphalia lenye idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani.

Janga lanyemelea

Kituo cha televisheni cha taifa cha jimbo la Bavaria BR kimesema watafuta hifadhi kadhaa wameachwa kulala kwenye mikeka mjini Munich wakati wa usiku wa kuamkia Jumapili baada ya mji mkuu huo wa jimbo kukaribia kutumbukia kwenye janga la kibinaadamu.

Polisi na wahamiaji wanaosubiri treni kuja Ujerumani kutoka Vienna Austria.
Polisi na wahamiaji wanaosubiri treni kuja Ujerumani kutoka Vienna Austria.Picha: imago/Eibner Europa

Polisi ya Munich imesema uwezo wao umefikia kikomo wakati maafisa wa serikali wakifikiria kuufunguwa uwanja uliotumika kwa michezo ya Olympiki mwaka 1972 kama kituo cha ziada cha kuhifadhi wahamiaji.

Kwa mujibu wa gazeti la Jumapili la Welt am Sonntag polisi wa shirikisho la Ujerumani BKA imeemewa na suala la ukaguzi wa vitambulisho na kuchukuwa alama za vidole kulikofikia 360,000 mwaka huu.

Michezo ya jeshi yaahirishwa

Jeshi la Ujerumani Bundeswehr limefuta michezo yake ya wanajeshi wa akiba ili kuwezesha kupatikana kwa vitanda 200 katika kambi yake ilioko kwenye mji wa kaskazini wa Bavaria wa Roth.

Wahamiaji mpakani mwa Hungary na Austria.
Wahamiaji mpakani mwa Hungary na Austria.Picha: picture-alliance/AP/R. Zak

Askofu wa Kiprotestanti wa Bavaria Heinrich Befdord -Srohm katika ujumbe alioutuma wakati wa usiku amewataka waumini kufunguwa vituo vya parokia zao katika jamii kuwapokea wakimbizi.

Baraza la kanisa la jimbo hilo linapanga kutowa euro milioni 20 kwa ajili ya matumizi ya dharura.Hapo Jumamosi Kansela Angela Merkel ameitaka Ugiriki ambayo bado inakabiliwa na matatizo yake yenyewe kuchukuwa hatua zaidi kulinda mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya na Uturuki.

Waziri wa Uchukuzi wa Ujerumani Alexander Dobrindt wa chama cha kihafidhina cha Christian Demokratik (CSU) cha Bavaria ameutuhumu Umoja wa Ulaya kwa kushindwa kabisa kulinda mipaka yake ya nje.Amesema ni muhimu kuchukuliwa kwa hatua zinazopasa hivi sasa ili kuzuwiya mmiminiko huo wa wahamiaji.

Repoti nyengine zenye kuzingatia duru zilizo karibu na mawaziri wa Ujerumani zinasema wasi wasi unaongezeka kwa vitisho vya usalama vya magaidi wanaotoka maeneo ya vita nchini Syria na Afrika Kaskazini kujipenyeza miongoni mwa wakimbizi.

Mazingira hatari kambi ya Röszke

Wafanyakazi wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka katika kambi ya wakimbizi wanaowasili Hungary iliozungushwa uzio kwenye mpaka na Serbia wamesema kambi hiyo yenye utata haina huduma za msingi za usafi na zana za matibabu.

Wahamaji na polisi karibu na kituo cha kupokea wahamaji cha Rozske nchini Hungary.
Wahamaji na polisi karibu na kituo cha kupokea wahamaji cha Rozske nchini Hungary.Picha: Reuters/Laszlo Balogh

Msemaji wa shirika hilo Sarah Schroeder amesema magonjwa ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka kutokana na kwamba kambi hiyo haina maji ya bomba na mahala pa kukoga.

Hungary inapanga kukaidi onyo la Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa na inaanzisha sheria mpya kuanzia Jumanne kuwashtaki kwa makosa ya jinai wahamiaji wapya wanaowasili kwenye uzio wake wa kilomita 175 ambao unaendelea kujengwa pamoja na watu wanaowasaidia wahamiaji hao.

Wakati Hungary ikifunga mpaka wake huo na Serbia kituo kipya cha kupitia wahamiaji hao kinaweza kuwa Croatia.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/AFP/DW

Mhariri : Isaac Gamba