Ujerumani yaikubali jinsia ya tatu
9 Novemba 2017Watu hao sasa watakuwa wanatambulika na jinsia nyengine mbali na mwanamume au mwanamke. Uamuzi huo wa mahakama uliotajwa kama wa kihistoria na shirika linalotetea masuala ya ubaguzi Ujerumani, unaashiria kutikiswa pakubwa kwa sera za jinsia katika nchi hii yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na haya yanajiri mwezi mmoja baada ya ndoa za jinsia moja kuhalalishwa.
Mahakama hiyo ya kikatiba ilitoa uamuzi wake kutokana na kesi ambapo mlalamikaji aliyetambuliwa kama Vanja na aliyezaliwa mwaka 1989, alikuwa anataka jinsia yake katika usajili wa kuzaliwa ibadilishwe kutoka mwanamke na iwekwe kama mtu aliye na jinsia mbili, ila maafisa walilikataa hilo kwa msingi kwamba sheria inakubali mtoto asajiliwe tu kama mwanamume au mwanamke au iwapo hilo halitofanyika basi, nafasi hiyo katika usajili isijazwe kabisa.
Mwanamume kaaida ana kromosomu X na Y
Mlalamikaji huyo alilalamika kwamba huo ni ukiukaji wa haki zake na katika mapambano ya miaka mitatu kortini, Vanja alitoa ushahidi wa viinitete ulioonesha kwamba ana kromosomu moja ya X ila hana ya pili ambapo kwa kawaida mwanamke anastahili kuwa na kromosomu mbili za X huku mwanamume akiwa na kromosomu moja ya X na moja ya Y.
Baada ya uamuzi huo, Vanja alikuwa na haya ya kusema.
"Sote tuna utambulisho wa aina fulani, jinsi tunavyojiona au jinsi tunavyojieleza," alisema Vanja. "Na kwa sababu nilikuwa nahisi kwamba hakuna maneno, nafasi wala watu ambao ni vielelezo vyema kwangu, nilikuwa na wakati mgumu wakati nilipokuwa nikikuwa."
Mahakama hiyo iliyoko katika mji wa magharibi wa Ujerumani, Karlsruhe, ilitoa siku ya mwisho ya sheria hiyo kubadilishwa kuwa mwishoni mwa mwaka ujao na imesema imefanya uamuzi wake kutokana na haki za mtu za kimsingi na haki yake ya kulindwa dhidi ya ubaguzi kama ilivyo katika katiba ya nchi hiyo.
Mtu mwenye jinsia mbili anaweza kuwa na viungo viwili vya utambulisho
Mahakama hiyo pia imesema kwa sasa korti na mamlaka za serikali hazistahili kuwalazimisha watu walio na jinsia mbili kutambulika kama wanawake au wanaume, jambo lililoungwa mkono na mtaalam wa masuala hayo Profesa Konstanze Plett.
"Imethibitishwa na mahakama ya kikatiba nchini kwa mara ya kwanza kwamba, kufanya jinsia ziwe mbili tu, ni jambo linalokiuka haki za wengine," alisema Plett. "Hii sio sawa kabisa kwa kuwa hata ikiwa walio katika hali hiyo ni wachache, haki za wachache zinastahili kuheshimiwa pia, sio lazima liwe suala la makundi ya watu wengi. Na hili limethibitishwa,"aliongeza Profesa huyo.
Kwa kawaida mtu anayetambulika kama aliye na jinsia mbili ni mtu ambaye hawezi kutambulika katika zile jinsia zilizozoeleka za mume na mke, kwa hiyo ni mtu ambaye huenda akawa na viungo ambavyo sio kamili vya kumtambulisha kama mwanamume au mwanamke au anaweza kuwa na viungo vyote kwa pamoja.
Serikali ya Ujerumani imesema itautii uamui huo wa mahakama huku msemaji katika wiara ya masuala ya ndani Johannes Dimroth akisema serikali iko tayari kuitekeleza sheria hiyo.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef