1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaisaidia Tume ya Uchaguzi Kenya

16 Januari 2013

Ujerumani imeisaidia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kwa vifaa vitakavyotumiwa na wananchi kujifahamisha utaratibu wa upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 4 Machi.

https://p.dw.com/p/17LB9
Die deutsche Botschafterin in Nairobi, Kenia Frau Margit Hellwig-Boette in Ihrer Residenz in Nairobi. Foto: DW-Korrespondent Alfred K. Nyale, 10.07.2011
Margit Hellwig-BoettePicha: DW

Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Bi Margit Hellwig-Boette, leo alasiri atakabidhi rasmi IEBC vifaa hivyo ambavyo ni mabango 85,000 na vijitabu vya maelezo 85,000 katika kituo cha IEBC cha Dandora mjini Nairobi.

Vifaa hivyo ambavyo ni mchango kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) vitawasaidia wapigakura nchini Kenya kuelewa vyema shughuli nzima ya upigaji kura kwenye uchaguzi ujao.

Shirika la GIZ linaunga mkono uchaguzi huru na wa amani nchini Kenya na linafanaya hivyo kupitia miradi miwili inayoendelea ya Uongozi Bora na Mpango wa Haki ya Kijamii.

Mbali na kutoa vifaa hivyo vya kuelimisha umma, shirika hilo pia linaunga mkono juhudi nyingine za kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki hasa katika Idara ya Mahakama kwa kushirikisha mabadiliko na matayarisho ya usuluhishaji mizozo ya uchaguzi.

Pia shirika la GIZ linasaidiana na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano kukabiliana na matamshi ya chuki wakati wa kampeni zinazoendelea za uchaguzi mkuu kwa ushirikiano na Tume ya Mawasiliano nchini na IEBC.

Vifaa hivyo vimetolewa siku moja kabla uteuzi wa vyama kufanyika hapo kesho kuwateua wagombea wa viti mbali mbali kwenye uchaguzi wa tarehe 4 Machi.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi

Mhariri: Josephat Charo