1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz apoteza kura ya imani bungeni

17 Desemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amepoteza kura ya imani bungeni jana jioni, hatua inayofungua njia ya kufanyika uchaguzi wa mapema Februari 23 ambao yumkini utahimisha utawala wake uliodumu kwa miaka minne.

https://p.dw.com/p/4oEB1
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture-alliance

Wabunge 394 kati ya 717 wa Bunge la Taifa, Bundestag, walipiga kura ya kutokuwa na imani na serikali ya Scholz huku 207 pekee ndiyo walimuunga mkono. Kufuatia matokeo hayo Scholu alimwomba Rais Frank-Walter Steinmeier kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi.

Kura hiyo ya imani bungeni inafuatia kusambaratika kwa serikali ya mseto Kansela Scholz  baada ya kiongozi huyo kumfuta kazi waziri wake wa fedha kutoka chama mshirika cha FDP kutokana na mabishano juu ya namna ya kufadhili bajeti ya mwaka ujao.

Uamuzi huo wa mwezi Novemba uliiweka rehani serikali ya Scholz anayetoka chama cha SPD na washirika wengine wa chama cha kijani, Die Grüne.

Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha umashuhuri wa Scholz umeporomoka na kuna uwezekano mkubwa kwa chama cha kihafidhina cha CDU cha Kansela wa zamani Angela Merkel kurejea madarakani.