1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa kulinda amani Sudan Kusini kuongezwa muda

Sylvia Mwehozi
13 Machi 2020

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kwa kauli moja limepiga kura ya kuongeza mamlaka ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.

https://p.dw.com/p/3ZLFn
UN Blauhelme Süd Sudan Südsudan
Picha: Getty Images/A.G.Farran

Hatua hiyo inakaribisha maendeleo ya kuridhisha kuelekea upatikanaji wa amani, na kupunguza ghasia za kisiasa kutoka pande zinazohasimiana.

Baraza hilo limezitaka pande zote katika mzozo huo kukomesha mapigano kwa haraka, na kushiriki kwenye mazungumzo ya kisiasa pamoja na kutekeleza makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano. Pia limetishia kuwawekea vikwazo "wale watakaochukua hatua za kudhoofisha amani, ustawi na utulivu nchini Sudan Kusini".

Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba taifa hilo lingekuwa na amani na utulivu mara baada ya kujipatia uhuru ilioupigania kwa muda mrefu kutoka taifa jirani la Sudan mwaka 2011. Lakini badala yake taifa hilo changa lilitumbukia kwenye machafuko ya kikabila Desemba 2013, wakati vikosi utiifu kwa rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka, vilipoanza kupigana na vile vya makamu wake Riek Machar wa kabila la Nuer.

Jitihada kadhaa za upatikanaji amani zilishindwa, ikiwemo mkataba ulioshuhudia Machar akirejea kama makamu wa rais mwaka 2016, kabla ya kuikimbia nchi miezi michache baadae. Mapigano ya kikabila yamewaua watu karibu 400,000 na wengine wapatao milioni moja kukosa makazi.

Baraza la usalama limesema kuanza kwa serikali ya umoja wa kitaifa ni "hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu". Aidha Umoja wa Mataifa "umepongeza hali ya maelewano na utashi wa kisiasa ulionyeshwa na pande zote katika kutengeneza mazingira ya kusonga mbele na mchakato wa amani."

USA David Shearer
David Shearer mjumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini Picha: picture alliance/ZUMAPRESS/A. Lohr-Jones

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani linaongeza mamlaka ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani hadi Mwezi Machi mwaka 2021 pamoja na kubakisha kiwango cha wanajeshi wake 17,000 na wafanyakazi wa polisi wa kimataifa wapatao 2,101.

David Shearer,ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini na alisema kwamba "hali ya usalama bado ni mbaya-bado kuna watu wenye silaha na tunatumai kwamba tunapaswa kuendelea na hatua inayofuata ya kuzileta pamoja pande zote, kuhakikisha wanawake na watoto wanarejea nyumbani kwao na wale waliotekwa nyara."

Lengo kubwa la ujumbe huo nchini Sudan Kusini ni kuwalinda raia, usambazaji wa misaada ya kiutu na kusaidia utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018. Hata hivyo baraza la usalama limeelezea "wasiwasi mkubwa " juu ya watu  karibu millioni 3.9 ambao hawana makaazi ndani ya nchi na mgogoro wa kiutu huku watu milioni 5.29 wakihofiwa kukabiliwa na "ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula".

Mshauri wa ujumbe wa Marekani Michael Barkin amelieleza Baraza la Usalama baada ya kura ya alhamis kwamba hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi ambapo mamlaka ya ujumbe huo, inaongezwa katika "muktadha wa maendeleo chanya".

Naibu balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa Jurgen Schulz, amehimiza utekelezwaji wa "majukumu muhimu" kwa watu wa Sudan Kusini ambao wataweza kufaidika na amani ya kudumu. Amesema Ujerumani imefurahishwa na azimio hilo kujumuisha athari mbaya za hali ya hewa, ambayo ilishuhudia uvamizi wa makundi ya nzige mwezi uliopita.