Juhudi za kufufua mazungumzo ya amani
25 Februari 2016Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameshawasili katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura,akiongoza ujumbe wa Umoja wa Afrika ulioamuliwa kuundwa viongozi wa Umoja huo walipokutana mwishoni mwa mwezi wa january uliopita mjini Addis Abeba. Mbali na rais Zuma,ujumbe huo wa Umoja wa Afrika unawaleta pamoja marais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz,Macky Sall wa Senegal,Ali Bongo Ondimba wa Gabon na waziri mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Dessalegn.
Mara baada ya kuwasili viongozim hao wa nchi tano za Umoja wa Afrika wamekwenda kuweka mashada ya mauwa kwenye makaburi ya wahanga wa demokrasia,ikiwa ni pamoja na lile la rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemkorasia nchini humo Melchior Ndadaye.
Kuwasili ujumbe huo wa viongozi wa mataifa ya Afrika mjini Bujumbura ni sehemu ya juhudi jumla za kidiplomasia za kujaribu kusaka ufumbuzi wa amani kwa mzozo wa Burundi.
Thibitisho la serikali kwa Ban Ki-Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban-Ki-Moon,ambae binafsi alikuwa zirani mjini Bujumbura jumatatu na jumanne wiki hii,alihakikisha kwamba amepatiwa thibitisho na rais Pierre Nkurunziza kwamba mjadala utakaozihusisha pande zote utaanzishwa nchini humo.
Juhudi za awali za majadiliano zilishindwa kwasababu serikali ya Burundi haikuwa ikitaka kuzungumza na baadhi ya vyama vya upinzani.
"Viongozi wa mataifa ya Afrika wanakuja kujadiliana na serikali pamoja na wahusika wengine kuhusu namna ya kuanzisha mdahalo wa pande zote," amesema mwanadiplomasia mmoja wa kiafrika aliyeko mjini Bujumbura na ambae hakutaka jina lake lijulikane.
Suala la wanajeshi wa Afrika halizungumziwi
"Mada ya kutumwa kikosi cha nchi za Afrika haimo katika ajenda ya mazungumzo" ameongeza kusema mwanadiplomasia huyo.
Umoja wa Afrika uliamua mwezi decemba mwaka jana kutuma kikosi cha wanajeshi 5000 nchini Burundi ili kuzuwia wimbi la matumizi ya nguvu. Lakini uamuzi huo ulikabiliwa na upinzani mkubwa wa rais Pierre Nkurunziza pamoja pia na viongozi kadhaa wa Afrika katika mkutano wao wa kilele mwezi Januari.
Burundi imetumbukia katika mzozo wa kisiasa na kugubikwa na matumizi ya nguvu tangu rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kugombea mhula wa tatu mwezi wa aprili mwaka 2015.
Matumizi ya nguvu yaliyofuatia yameangamiza maisha ya zaidi ya watu 400 na zaidi ya 240.000 kuihama nchi hiyo. Mashirika yanayopigania haki za binaadamu yanazungumzia kuhusu kuwepo makaburi ya jumla,visa kadhaa vya watu kuuliwa kiholela,mauwaji yaliyolengwa na kudai ufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu madai hayo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman