1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukweli badala ya hisia: Ripoti ya wahamiaji ya Malteser

29 Septemba 2017

Ripoti 11 za ujumuishwaji wa wageni zimetolewa na serikali ya Ujerumani, ambapo ya mwishoni kabisa ilikuwa ni matokeo ya idadi kubwa ya wakimbizi, lakini sasa jumuiya ya misaada  ya Kanisa Katoliki inatoa yake yenyewe.

https://p.dw.com/p/2kzLo
Symbolbild Deutschland Flüchtlinge werden in Friedland erwartet
Picha: picture-alliance/dpa/S. Rampfel

Ripoti nyengine ya wahamiaji? Karl Prinz zu Löwenstein wa shirika la huduma za kiutu la Kanisa Katoliki la Malteser anashuku endapo suali hili linaweza kuulizwa. Ndio maana, hapo Jumatano (27 Septemba) alielezea kwa nini shirika lake linawasilisha ripoti yake lenyewe kwa mara ya kwanza: kwa sababu ni ya kipekee, anasema kamishna huyo wa ripotiya wahamiaji ya Malteser. Lakini hakuwakuwa na makusudi ya kushindana na wengine.

Ugunduzi wa ripoti hiyo, ambao umekusanywa kwenye kurasa 112, ni matokeo ya chambuzi za kisayansi juu ya suala la uhamiaji kwa upande mmoja na kile kilichopatikana kutokana na uzoefu wa muda mrefu wa shirika hilo katika kuwasaidia wakimbizi. 

Kimsingi, Prinz zu Löwenstein ana wasiwasi na namna mjadala kuhusu wahamiaji unavyoweza kuwa zaidi kuhusu hisia. Ndio maana ripoti hii imepewa jina la "ukweli badala ya hisia" – ambapo, hata hivyo, anakiri kwamba hisia hizo sio mbaya moja kwa moja.

Kutolewa mara tu baada ya uchaguzi si bahati mbaya

"Nani ambaye hataguswa na majaaliwa ya watu wenye uhitaji?" Anauliza kamishna huyo wa Maltese. Hata hivyo, watu wengi wanaweza pia kuchukuliwa na hisia kali "linapokuja suala la khofu za kutengwa." 

Symbolbild - Flüchtlinge
Idadi ya wakimbizi wengi walioingia Ujerumani baina ya mwaka 2015 na 2016 imechochea mjadala mkubwa kuhusu hadhi na nafasi yao.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Ukweli kwamba ripoti hiyo imetolewa muda mchache baada ya uchaguzi mkuu nchini Ujerumani si jambo la bahati mbaya. Imechapishwa hasa kwenye muda huu ili kuvutia "maamuzi ya kisiasa" kwa wabunge wapya, kwa mujibu wa taarifa kwa waandishi wa habari iliyoambatanishwa na ripoti yenyewe.

Taasisi ya Walter Eucken yenye makao yake mjini Freiburg inahusika na sehemu ya kisayansi ya ripoti hii. Mkurugenzi wake, Lars Petersfeld, anaanza dibaji yake kwa kukumbushia kwamba "Ujerumani ni na ilikuwa nchi ya wahamiaji." 

Kwa hili, mtu wala hapaswi hata kugeuka nyuma sana kwenye historia, bali anaweza tu kuchunguza kwa kuangalia vipindi tafauti vya majilio ya wakimbizi na wahamiaji tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Uzoefu unaopatikana unaonesha kwamba “ushiriki kwenye soko la ajira“ ni nyenzo muhimu kwa mafanikio ya ujumuishwaji wageni kwenye jamii ya Kijerumani, anasema Feld.

Nakisi ya sifa miongoni mwa wahamiaji

Infografik Ausgaben für Flüchtlinge ENG

Juu ya yote, wahamiaji kutoka mataifa yasiyokuwa ya Ulaya hawajajumuishwa vyema kwenye soko la ajira la Ujerumani, anasema mtafiti huyo wa masuala ya uhamiaji. Anataja miongoni mwa vikwazo vikubwa kabisa ni uwezo wa lugha, ukosefu wa mafunzo, na matatizo yanayohusiana na kutambuliwa kwa viwango vyao vya elimu.

Ikiwa tunaangalia kwa undani uhamiaji wa wakimbizi kwa mwaka 2015/2016, ni jambo linalotegemewa kwamba "watu hawa wanastahiki zaidi kubakia kwa sababu ya msaada na sio elimu yao ya juu kwa sababu ya elimu na sifa zao."

"Kadiri kasi ya kuwajumuisha kwenye soko la ajira inavyokuwa kubwa, ndivyo mafanikio ya ujumuishwaji yanavyokuwa makubwa pia," anasema mkuu wa utafiti huo.

Feld anapendekeza pia kuwepo kwa mtazamo wa kina juu ya namna neno "uhalifu" linavyochukuliwa na watu kupandisha hisia kali dhidi ya wageni. Kiujumla, hivi leo nchini Ujerumani, kiwango cha uhalifu ni kidogo zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 20 nyuma. 

Lakini idadi ya washukiwa wenye asili ya kigeni imeongezeka kutoka mmoja kwa kila washukiwa watatu mwaka 1993 hadi asilimia 40 mwaka 2016. 

Hata hivyo, kwenye takwimu hizi munajumuishwa pia uvunjaji wa haki za kuomba hifadhi au mambo yaliyo mageni, makosa ambayo Wajerumani hawawezi kuyatenda kamwe.

Uhalifu: Tafauti kubwa kwenye mataifa asili

Infografik Tatverdächtige unter Zuwanderern ENG

Mtu hawezi tu kudai kuwa "uhamiaji wa wakimbizi umekuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa uhalifu ndani ya kipindi cha miaka miwili hii," anasema Feld. 

Hata hivyo, kuna baadhi ya tafauti za kimsingi kati ya nchi za asili. Kwa mfano, asilimia 11 ya washukiwa wasio Wajerumani wanatoka mataifa ya kaskazini mwa Afrika, lakini wao ni asilimia mbili tu ya wahamiaji wote. 

Kwa upande mwengine, wahamiaji kutoka Syria, Iraq na Afghanistan, kutokana na idadi yao, wanajikuta wakiwa wachache zaidi kwenye adhabu kuliko wale wa mataifa mengine.

Akizungumzia suala la ukombo wa uwezo wa kupokea wakimbizi, Feld anasema hafikirii kuwa hilo ni jambo zuri. "Hili lilikuwa jambo la aibu", anasema Feld, ingawa Prinz zu Löwenstein anazungumzia ufanisi wa sera hiyo ya kuweka ukomo.

Ama ikiwa taasisi hii ya Kikatoliki itaendelea kufuatilia kwa kina masuala haya ya wakimbizi ama la, bado ripoti yao inaonesha wazi kuwa uhamiaji bado ni changamoto kwa jamii ya Ujerumani.

Kwa hivyo, kwa kutumia uzoefu wao wa miaka mingi kwenye suala hili, wanakusudia kuchangia kwenye mdahalo huu kwa kutoa ukweli ulivyo, na sio hisia pekee.

Mwandishi: Marcel Fürstenau/DW
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf