1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kufunga kambi tano DRC

Daniel Gakuba
21 Julai 2017

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, kimetangaza kuzifunga kambi tano katika mkoa wa Kivu Kaskazini, sambamba na mpango wa kupunguza walinda amani nchini humo.

https://p.dw.com/p/2gwOW
Beni Demokratische Republik Kongo Blauhelmsoldaten 23.10.2014
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwepo DRC kwa zaidi ya miaka 20Picha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Hatua hiyo ya kupunguza idadi ya wanajeshi wa Kikosi cha MONUSCO ilitangazwa na kamanda wa kikosi hicho Jenerali Bernard Commins, katika mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki. Jenerali Commins alisema kambi hizo tano zitafungwa katika maeneo ambayo wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwepo kwa zaidi ya miaka 20.

''Mkoa wa Kivu Kaskazini ni eneo lenye umuhimu mkubwa katika mchakato wa kulinda amani, likiwa na brigedi nzima na vikosi vingine vya msaada. Tutafunga kambi katika wilaya kadhaa; mbili katika wilaya ya Walikale, mbili nyingine katika wilaya ya Masisi, na kambi moja katika wilaya ya Lubero. Haya ni kulingana na wajibu wetu wa kutekeleza maagizo ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa'' Amesema Jenerali Commins.

Hakutaachwa pengo la ghasia mpya

Wengi wa wanajeshi 16,000 wa kikosi cha MONUSCO wamepelekwa Kongo kupambana na makundi ya waasi yenye silaha, ambayo yamekuwa yakisababisha msururu wa migogoro, Baadhi yao huwasindikiza wanavijiji wanapokwenda sokoni hususan katika mkoa wa Kivu Kaskazini, na huwapa sehemu salama ya kuishi, wanapokimbia ghasia za makundi ya waasi katika maeneo wanamoishi.

Kongo Lusenda MONUSCO Flüchtlingslager burundische Flüchtlinge
Ghasia zinazosababishwa na makundi yenye silaha zimewafanya maelfu ya watu kuyahama makazi yao Mashariki mwa KongoPicha: MONUSCO/Abel Kavanagh

Kamanda wa Kikosi cha MONUSCO amesema kufunga kambi zao katika maeneo hayo hakuepukiki, na kuongeza kuwa mchakato huo unaendeshwa katika mtindo ambao utahakikisha kwamba pengo watakaloliacha baada ya kufunga kambi zote, halitatumiwa kuanzisha vurugu mpya.

Wanavijiji waingiwa na hofu

Kuvuja kwa taarifa za kufungwa kwa kambi za walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa kumesababisha maandamano ya raia katika maeneo husika, ambao wanahofu kwamba makundi yenye silaha yatarejea kuviteka vijiji vyao.

Hata mbunge Juvenal Munobu Mubi ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ulinzi katika Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amesema kufungwa kwa kambi hizo za MONUSCO kumefanywa kwa wakati usiofaa.

Angola flüchtchtlings Kinder aus Kongo
Mkoa wa Kasai umekuwa uwanja mpya wa ghasia nchini DRCPicha: UNICEF/N. Wieland

Monubu amesema, ''Kimsingi, ni jukumu la jeshi la serikali na polisi kulinda usalama wa nchi, lakini kwa sababu hatujaweza kukamilisha mabadiliko katika mfumo wetu wa usalama, bado tunahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa, lakini kwa kuzingatia kuwa MONUSCO ndio ujumbe mkubwa zaidi wa kulinda amani duniani, maoni yangu ni kwamba Umoja wa Mataifa haukupaswa kuzifunga kambi zake katika maeneo hayo''.

Kamanda wa MONUSCO, Jenerali Bernard Commins amesema watafungua kambi mpya katika mkoa wa Kasai ulioko katikati mwa nchi, ambao umeshuhudia machafuko mnamo miezi ya hivi karibuni. Maelfu ya raia katika mkoa huo wameyapa kisogo makazi yao, wakikimbia ghasia hizo. Wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa waliuawa katika mkoa huo, mapema mwaka huu.

Mwandishi: Patrice Chitera/DW Africalink

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Mohammed Khelef