1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kuhusu uhalifu wa kivita Ituri, DRC

John Juma Mhariri: Sekione Kitojo
28 Mei 2020

Umoja wa Mataifa umesema kuna uwezekano kwamba visa vya uhalifu dhidi ya ubinadamu pamoja na uhalifu wa kivita vilitendeka kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kutokana na matendo ya watu kuuawa.

https://p.dw.com/p/3csqW
Picha: Getty Images/AFP/L. Healing

"Matendo ya watu kuuawa, kuchinjwa, kubakwa na visa vingine vya kikatili vilifanywa na wanamgambo hasa kutoka jamii ya kabila la Walendu kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo''. Imesema ofisi ya Umoja wa Mataifa.

Kwenye ripoti yake iliyotolewa Jumatano, Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) imesema kwamba kati ya mwezi Novemba hadi Aprili mwaka huu, ikiwa ni jumla ya miezi sita, watu wasiopungua 296 waliuawa. 151 walijeruhiwa na 38 walibakwa wakiwemo wanawake pamoja na watoto. Visa hivyo vilitendwa hasa na wanamgambo wanaohusishwa na kundi la waasi la CODECO.

Wapiganaji wa kundi hilo hutoka katika kabila la Walendu.

Machafuko ya kikabila Ituri

Mkoa wa Ituri ulioko kaskazini mashariki mwa Congo, una utajiri mkubwa wa maliasili kama madini ya dhahabu, almasi na mafuta.

Mkoa huo uliwahi kukumbwa na mapigano mabaya zaidi ya kikabila kati ya mwaka 1999 na mwaka 2007, baada ya mvutano wa mamlaka au kupigania udhibiti wa eneo hilo kati ya makundi ya waasi, wengi kutoka jamii ya Wahema na Walendu.

Baada ya miaka kadhaa ya kuwepo utulivu, mzozo wa ulipizaji kisasi ulizuka tena mnamo Disemba 2017, na hivyo kufufua uhasama wa muda mrefu kuhusu umiliki wa ardhi.

Ripoti ya UNJRHO imeongeza kuwa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia hayakuyalenga tu makabila ya Hema na Alur, bali pia yalizilenga jamii ambazo awali hazikuwa sehemu ya machafuko.

Mizozo ya miaka kadhaa ya makundi yenye silaha mkoa wa Ituri imesababisha mauaji ya watu wengi huku zaidi ya watu milioni 1.2 wakiyakimbia makaazi yao.
Mizozo ya miaka kadhaa ya makundi yenye silaha mkoa wa Ituri imesababisha mauaji ya watu wengi huku zaidi ya watu milioni 1.2 wakiyakimbia makaazi yao.Picha: AP

Mapigano katika maeneo ya uchimbaji madini

Makabiliano yalichacha zaidi kuanzia mwezi Machi mwaka huu hususan katika maeneo ya kiufundi na yanakochimbwa madini.

Ofisi ya UNJRHO imesema kwamba, kuendelea kwa machafuko hayo kunaweza kuwalazimisha watu wa jamii zinazolengwa na ambao hadi sasa zimeonyesha kujiepusha na mashambulizi hayo, kuunda makundi ya wanamgambo ili kujilinda wenyewe. Hali ambayo inauwezo mkubwa wa kuchochea vita zaidi kati ya makabila katika eneo hilo.

Tangu Juni mwaka 2018, maelfu kwa maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makaazi yao, na hivyo kufanya idadi ya wakimbizi kutoka mkoa wa Ituri kuzidi milioni 1.2. Hayo ni kwa mujibu wa UNJRHO.

Mvutano wa ndani kwa ndani CODECO

Mnamo Machi 25, kiongozi wa kundi la waasi la CODECO Justin Ngudjolo aliuawa kufuatia shambulizi la kushtukiza, hali iliyosababisha mvutano wa kung'ang'ania uongozi na pia kugawika kwa kundi hilo.

Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UNJRHO, imesema kuwa kuna hatari kubwa kwamba viongozi wenye misimamo mikali wataibuka na kulitumbukiza eneo hilo katika machafuko mabaya yasiyokwisha dhidi ya jeshi na pia dhidi ya raia.

Chanzo: RTRE