Umoja wa Ulaya na Afrika: Mkutano wa kilele walenga ajira
29 Novemba 2017Zaidi ya viongozi 80 wa Afrika na Ulaya wanakutana leo-Jumatano Abidjan, Cote de' Ivoire kwa lengo la kukuza ajira na kuimarisha utulivu kwa wananchi wa Afrika ambao idadi yao inaongezeka, huku wengine wakitaka kuanzishwa kwa mpango mpya kwa ajili ya maendeleo barani Afrika ''Marshall Plan''.
Mkutano huo wa kilele wa siku mbili unaanza wakati ambapo Umoja wa Ulaya unazidi kuona kuwa hatma yake inafungamana na Afrika, kutokana na suala la uhamiaji lisilo la kawaida pamoja na mashambulizi ya kigaidi.
Pia unafanyika wakati ambapo China, India, Japan mataifa ya Ghuba ya Kiarabu na mataifa mengine yanashindana kwa ushawishi katika bara ambalo nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya zinabakia kwa ujumla zenye uchumi mkubwa na mchangiaji wa kisiasa. Spika wa Bunge la Ulaya, Antonio Tajani amesema Afrika itahitaji kubuni mamilioni ya ajira ili kuwakaribisha wageni katika soko la ajira.