UN: Jeshi la Congo lilifukua makaburi ya pamoja
26 Julai 2017Ripoti ya pamoja ya ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Congo UNJHRO ni ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kupendekeza moja kwa moja kwamba vikosi vya serikali vilichimba makaburi hayo. Waziri wa haki za binadamu wa Congo hakupatikana mara moja kujibu tuhuma hizo lakini serikali mara kadhaa imekanusha vikosi vyake kuhusika na makaburi ya halaiki yaliyogunduliwa tangu wanamgambo wa Kaimuna Nsapu walivyoanzisha uasi dhidi ya serikali mwezi agosti na kuwataka wanajeshi wa serikali kuondoka eneo hilo.
Ripoti hiyo inasema " kuanzia Juni 30 mwaka huu, UNJHRO imetambua jumla ya makaburi ya pamoja 42 katika majimbo matatu ya Kasai, mengi yake huenda yamechimbwa na jeshi la Congo kufuatia mapambano na wanachama wanaosadikiwa kuwa wanamgambo."
Mapema mwezi huu ofisi hiyo ilisesema kwamba imebaini makaburi mengine 38 ya halaiki katika eneo la magharibi mwa Kasai, na kufanya jumla ya makaburi hayo kufikia 80. Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujaric alisema kuwa, "ofisi ya haki za binadamu na ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaelezea utayari wake kuunga mkono mamlaka ya DRC kuangazia uhalifu uliofanywa Kasai na mapambano dhidi ya wale wanaofanya makosa bila ya kuchukuliwa hatua."
Watu zaidi ya 3000 wameuawa na wengine milioni 1.4 kukosa makazi katika vurugu, ikiwa ni sehemu ya ongezeko la machafuko katika nchi hiyo tangu rais Joseph Kabila alivyokataa kuondoka madarakani baada ya kumalizika kwa muhula wake mwezi desemba.
Vurugu hizo zimesababisha hofu ya kuzuka kwa mgogoro mkubwa katika nchi hiyo ya Afrika ya kati, ushindani wa kikabila na ushindani wa rasilimali za madini. Mamilioni ya raia waliuawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1996-2003, zaidi kwasababu ya njaa na maradhi.
Serikali inawatuhumu wanamgambo kuhusika na makaburi ya halaiki na pia inadai kwamba baadhi ya maeneo ambayo yaliyotambuliwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa yamekutwa hayana miili ya watu.
Pia inakanusha madai ya Umoja wa Mataifa kwamba wanajeshi wake kiutaratibu, wametumia nguvu za kupita kiasi ingawa mwezi huu mahakama iliwahukumu wanajeshi saba kwa kuwaua wanachama wanaoshukiwa kuwa wanamgambo katika mauaji ya pamoja yaliyopatikana katika mkanda wa vidio.
Umoja wa Mataifa umewateua wataalamu watatu wa haki za binadamu leo kuongoza uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na mauaji na uhalifu mwingine katika jimbo la Kasai katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, hatua ambayo inaweza kuleta mvutano na serikali. Congo inasisitiza kwamba mfumo wake wa sheria unaendesha uchunguzi wakati Umoja wa mataifa ukitoa msaada wa kitaalamu ama usafiri. Baadhi ya mataifa ya magharibi na makundi ya wanaharakati wamesema walikuwa na matumaini ya Umoja wa Mataifa kuwa na mamlaka makubwa zaidi.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga