1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yahimiza uchaguzi wa amani, haki DRC

14 Agosti 2018

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepongeza uamuzi wa Rais Joseph Kabila kutowania muhula mwingine katika uchaguzi ujao wa DRC, na kusema uchaguzi huo unapaswa kupelekea makabidhiano ya amani ya madaraka.

https://p.dw.com/p/3388x
UN-Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/Photoshot/Li Muzi

Baraza hilo pia limevihimiza vyama hasimu vya siasa nchini humo, pamoja na taasisi zinazohusika na maandalizi ya uchaguzi huo wa mwezi Desemba, kuhakikisha kuwa zoezi la upigaji kura linakuwa la amani na la kuaminika.

Baraza hilo ambalo ndiyo chombo chenye nguvu zaidi ndani ya Umoja wa Mataifa kilitoa taarifa jana Jumatatu na kukaribisha hatua za karibuni katika mchakato wa uchaguzi, ikiwemo ya Rais Joseph Kabila kutimiza ahadi yake ya kuheshimu katiba ya Congo kwa kutowania muhula wa tatu.

Wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa waliwahimiza washiriki wote kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya uwazi, uaminifu na ushirikishwaji. Walisema kuheshimu haki za msingi na kusimamia kalenda ya uchaguzi ni mambo muhimu yatakayohakikisha uchaguzi wa amani hapo Desemba 23.

DRC Präsident Joseph Kabila
Rais wa DRC Joseph Kabila.Picha: Reuters/K. Katombe

Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, alionekana kusalimu amri kwa shinikizo la kimataifa wiki iliyopita, wakati muungano wake tawala ulipomteuwa Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea wake wa nafasi ya rais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Shinikizo la kimataifa

Marekani, Ufaransa na Uingereza zilikuwa zimemuomba Kabila kubainisha wazi kwamba hatowania muhula mwingine, mnamo wakati kukiwa hofu kwamba kushindwa kwake kuachia madaraka kungeweza kusababisha vurugu.

Baraza pia limeihimiza tume ya uchaguzi kuhakikisha kwamba maombi yoyote ya msaada wa ugavi na usafirishaji pamoja na ufundi kwa ajili ya uchaguzi huo kutoka kwa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO, yanafanyika katika wakati.

Lakini Emerie Damien Kalwira, rais wa muungano unaopigania mpito nchini Congo anasema mazingira ya sasa hayatowi nafasi kwa uchaguzi huru na wa haki, na kusisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kishinikiza kuundwa kwa serikali ya mpito bila Kabila, ambayo itaandaa uchaguzi huru.

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo haijawahi kuwa na mabadilishano ya amani ya madaraka tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960. Baraza la Usalama linapanga kufanya ziara nchini humo kabla ya uchaguzi, na huenda ziara hiyo ikafanyika mwezi Oktoba.

Kongo Impfung gegen Ebola in Mbandaka
Congo imeanza kutumia tiba ya majaribio ya Ebola mashariki mwa nchi hiyo.Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Congo yaanza kutumia tiba ya majaribio ya Ebola

Wakati huo huo, wizara ya afya Congo imearifu kuwa wameanza kutumia tiba ya majaribio ya Ebola ya mAb114, kwa wagonjwa mashariki mwa nchi, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa dawa hiyo kutumika katika mripuko unaoedelea.

Tiba ya mAb 114 ilitengenezwa nchini Marekani na taasisi ya taifa ya afya kwa kutumia kinga za mwili za manusura wa mripuko wa Ebola katika mji wa magharibi mwa Congo wa Kikwit mwaka 1995. Ilionesha ufanisi wa asilimia 100 baada ya kujaribiwa kwa kima.

Wizara hiyo ya afya imesema mripuko wa sasa ulioanzia kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini umesambaa katika mkoa jirani wa Ituri, ambako mtu aliethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo alifariki baada ya kurejea nyumbani kutoka mji wa Mangina katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre,afpe

Mhariri: Josephat Charo