UN yaitaka DRC kutangaza kalenda ya uchaguzi
20 Septemba 2017Mkutano huo uliofanyika pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na ulioitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Amina Mohammed, ulihudhuriwa pia na ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Uingereza, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC, Jumuiya ya Nchi za Afrika ya Kati, na Kongo yenyewe.
Lengo lilikuwa ni kuja na mtazamo wa pamoja wa wadau wote kuelekea uchaguzi wa amani na wa kidemokrasia nchini Kongo.
Maman Sidikou, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, amesema mkutano huo umeiomba tume huru ya uchaguzi kutangaza haraka iwezekanavyo ratiba ya uchaguzi.
"Ni muhimu makubaliano ya kisiasa yaendelee kuheshimika, na tuelekee kwenye uchaguzi wa wazi na wa kidemokrasia utakaohakikisha mageuzi nchini Kongo. Kinachosubiriwa kwa hamu ni kutangazwa kwa kalenda ya uchaguzi ili kuweko na uchaguzi nchini Kongo."
Umoja wa Mataifa umesisitiza pia kutekelezwa kwa Makubaliano ya Kisiasa ya Desemba 31 kwa nia njema, ambayo yanataka pawepo na hatua za kuwahakikishia wapinzani uhuru wa kujieleza na vile vile kuheshimu haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa umeahidi uungwaji mkono wake kwa ajili ya kufanikisha taratibu za uchaguzi nchini Kongo.
Hata hivyo, serikali ya Kongo inasema kuchelewa kwa uchaguzi si kwa makusudi, bali kuna sababu zake, huku pakiwa na wasiwasi kuwa huenda kwa mara nyingine ukaahirishwa. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Kongo Lambert Mende ameondoa hofu hiyo.
"Kalenda hiyo ya uchaguzi haingetangazwa kabla ya masharti kadhaa kukamilika, kama vile kuwepo kwa kamati ya kitaifa ya ufuatiliaji wa makubaliano na vile vile daftari ya wapigakura. Hivi sasa masharti hayo yamekamilika na hakuna kitakachozuwiya kutangazwa kwa kalenda hiyo."
Upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu vinaendelea na kampeni yak e ya kuomba kueko na uchaguzi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Felix Tshisekedi na Moise Katumba wapo pia hapa NewYork katika juhudi za kueko na ufumbuzi wa mzozo wa Kongo.
Ni Saleh Mwanamilongo/DW NewYork
Mhariri: Mohammed Khelef