1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yalaani machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati

8 Juni 2021

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeitolea mwito Jamhuri ya Afrika ya Kati  na vikosi vyote vilivyoko katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro kuhakikisha usalama wa walinda amani wa Umoja huo

https://p.dw.com/p/3ua6J
Zentralafrikanische Republik Gedenken für getötete UN Soldaten in Bangui
Picha: UN/RCA

Wito wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usalama wa walinda amani wa Umoja huo umeonesha kama uliotolewa kutokana na wasiwasi wa kuwepo wanajeshi wa Urusi katika nchi hiyo  wanaoelezwa kuwa wanatowa mafunzo. Katika tamko lililoidhinishwa kwa sauti moja wakati wa kikao cha faragha kilichoongozwa na Ufaransa,wanachama wote wa nchi 15 za baraza hilo pia walitowa mwito kwa vikosi vya jamhuri ya Afrika ya Kati,wanajeshi wa kulinda amani na wengineo kushirikiana katika juhudi zao.

Hisia za Urusi kutoa mafunzo ya kijeshi Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Baraza hilo halikutaja vikosi vingine lakini inaonesha lilikuwa moja kwa moja likikusudia wanajeshi wa Urusi walioko nchini humo kama watoa mafunzo au waelekezaji wasiokuwa na silaha. Mashahidi mbali mbali na mashirika yasiyokuwa ya kiraia wamefahamisha kwamba watoa mafunzo hao wa Urusi ni wanajeshi wa kikosi maalum kutoka kampuni binafsi ya  kijeshi ya Wagner ambayo inahusika katika harakati nyingi za mapambano dhidi ya waasi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,ikishirikiana na wanajeshi wa kikosi maalum kutoka Rwanda na walinda amani wa Umoja wa Mataiafa.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pia halieleza ni kitu gani kilichosababisha kuitisha mkutano huo wa ghafla kuhusu suala hilo la Jamhuri ya Afrika ya Kati bali limesema kwamba mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja huo huenda yakaangaliwa kama uhalifu wa kivita.Mwanadiplomasia mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA umekuwa ukiandamwa na vizingiti vingi na kushambuliwa na vyombo vya habari katika nchi hiyo.Mwishoni mwa mwezi Mei,Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya amani,Jean-Pierre Lacroix aliyeitembelea nchi hiyo,aligusia kuhusu matukio ambayo yaliwahi kutokea  baina ya walinda amani na vikosi vingine lakini bila ya kutowa maelezo mengine ya kina.

Baraza la usalama la laani ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Zentralafrikanische Republik UN Soldaten in Bangui
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa BanguiPicha: UN/RCA

Wanachama wa baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao hicho walikabidhiwa  taarifa ya mkuu wa ujumbe wa  MINUSCA  Mankeur Ndiaye lakini hakuna maelezo yaliyowekwa wazi kwa umma juu ya taarifa hiyo. Hata hivyo tamko la baraza hilo imeweka wazi kwamba wanachama wote wanalaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kulinda ubinadamu katika nchi hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati,na kusisitiza juu ya haja ya kuwafikisha mbele ya sheria watuhumiwa.Kadhalika tamko hilo limezitaka pande zote kuheshimu majukumu yao chini ya sheria ya kibinadamu ya Kimataifa na kuhakikisha msaada wa kiutu unaruhusiwa kuingizwa kwa usalama na bila vizuizi.

Ikumbukwe kwamba siku ya Jumatatu Ufaransa ambayo ni koloni la zamani la Jamhuri ya Afrika ya Kati ilisimamisha msaada wake na ushirikiano wa kijeshi na serikali ya nchi hiyo iliyoko mjini Bangui ikiiwashtumu maafisa wa nchi hiyo kuwa sehemu ya wanaofanya kampeini  inayoongozwa na Urusi ya kuipaka matope Ufaransa.

Nchi hiyo ya Ufaransa inakabiliwa na shinikizo kubwa kwa muda ikitakiwa kuondowa vikwazo vya  silaha dhidi ya  Jamhuri ya Afrika ya Afrika,vikwazo ambavyo iliviweka tangu mwaka 2013 na vinavyomalizika Julai 31.

Katika barua ya hivi karibuni iliyoandikiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na Angola na ´Jamhuri ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati,iliyochapishwa jana na Umoja wa Mataifa,nchi hizo kwa mara nyingine zilitowa mwiti wa kufanyika mkutano maalum ukilenga kutafuta njia ya kuondolewa vikwazo hivyo vya Ufaransa.

Chanzo AFP