UN: Pande hasimu Sudan Kusini kutekeleza mkataba wa amani
7 Novemba 2019Taasisi hiyo muhimu zaidi ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa inayoelezea wasiwasi wake, baada ya wajumbe wake kufika ziarani hivi karibuni nchini humo na kushindwa kuona maendeleo yoyote makubwa katika kutekeleza vifungu muhimu vya makubaliano hayo ya amani yaliyosainiwa mwaka mmoja uliopita.
Kulingana na mkataba huo, kiongozi wa upinzani Riek Machar anapaswa kurejea katika mji mkuu Juba Novemba 12, na kukabidhiwa akwa mara nyengine tena wadhifa wa makamu wa rais Salva Kiir, hiyo ikiwa sehemu ya kugawana madaraka ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimedumu kwa miaka mitano na ambavyo vimesababisha vifo vya takriban watu 400,000, na mamilioni wakiachwa bila makao.
Mnamo Oktoba 20, Machar alikutana na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Juba na akaonya kuwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka uliopita yanaweza kuvunjika ikiwa serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa kama ilivyokubaliwa Novemba 12.
Badala yake anataka muda wa kuunda serikali hiyo urefushwe.