1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

UN yatoa wito wa kushughulikia mzozo wa Sudan

2 Desemba 2024

Tom Fletcher ambaye anahusika na masuala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, ametoa wito wa hatua za haraka za kimataifa kuchukuliwa kukabili mzozo unaozidi kuongezeka nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/4ndO0
Chad | Wahamiaji
Takriban watu milioni 26 ikiwa ni karibu nusu ya wakazi wa Sudan, wanakabiliwa na kitisho cha njaaPicha: Sam Mednick/AP

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaehusika na masuala ya kibinadamu ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka za kimataifa kukabiliana na mzozo unaozidi kuongezeka nchini Sudan, akiangazia hasa mateso ya mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro.

Tom Fletcher amezungumza na wakimbizi wakati wa ziara yake ya siku tisa katika nchi za Sudan na Chad, na kuapa kuweka wazi madhila yao na kuzitaka nchi zote duniani kutoa msaada zaidi.

Fletcher amesisitiza kuwa takriban watu milioni 26 ikiwa ni karibu nusu ya wakazi wa Sudan, wanakabiliwa na kitisho cha njaa huku pande zote mbili zinazopigana zikishutumiwa kutumia njaa kama silaha ya vita.

Sudan imekumbwa na vita tangu Aprili mwaka 2023, kati ya jeshi la taifa linaloongozwa na Abdel-Fattah al-Burhan na vikosi vya RSF, vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo.

Vurugu hizo zimesababisha vifo vya makumi ya maelfu watu na kuwafanya zaidi ya wengine milioni 11 kuwa wakimbizi. Umoja wa Mataifa unauelezea mzozo huo kuwa janga baya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni.