1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Mataifa ya Magharibi yanahusika na shambulio Crimea

27 Septemba 2023

Wizara ya Mambo ya Nje Urusi imewashutumu washirika wa Magharibi wa Ukraine, kwa kuisadia nchi hiyo kupanga na kufanya shambulio la wiki iliyopita dhidi ya kamandi ya jeshi la majini la Urusi katika bahari nyeusi.

https://p.dw.com/p/4Wsyz
Msemaji Wizara ya Mambo ya Nje Urusi Maria Zakharova
Msemaji Wizara ya Mambo ya Nje Urusi Maria ZakharovaPicha: SNA/IMAGO

Kulingana na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Urusi, Maria Zakharova, hapana shaka shambulio hilo lilipangwa zamani kwa kutumia taarifa za kijasusi, satelaiti za Jumuiya ya kujihami NATO na ndege za kijasusi.

Zakharova, amedai ushauri wa mipango yote ilitoka kwa taasisi za usalama za Marekani na Uingereza wakiwa katika ushirikiano mubwa na Ukraine. 

Moscow imekuwa ikirejelea usemi wake kwamba Marekani na washirika wa NATO wanaendelea kuhusika katika mgogoro wake na Ukraine kwa kutoa silaha kwa jirani yake huyo na pia kuisaidia na taarifa za kijasusi na kusaidia pia kupanga mashambulio dhidi ya vituo kadhaa vya Urusi.

Soma pia:Urusi:Marekani na Uingereza wanahusika na shambulizi Crimea

Ripoti ambazo hazijathibitishwa zinasema kwamba makombora kadhaa yaliyotolewa kwa Ukraine kama msaada na Uongereza na Ufaransa yalitumiwa katika shambulio hilo la Crimea. 

Hata hivyo wizara ya ulinzi ya Uingereza haikutoa tamko lolote juu ya mdai hayo, yaliyokuja siku moja baada ya vidio iliyomuonesha kamanda wa meli iliyoshambuliwa katika bahari hiyo Viktor Sokolov akiwa hai licha ya madai ya Ukraine bila ya kutoa uthibitisho kusema alikuwa miongoni mwa maafisa 34 waliouwawa katika shambulio hilo la siku ya Ijumaa katika mji wa bandari wa Sevastopol.

Mfululizo wa mashambulizi Crimea

Rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Urusi kutoka kwa Ukraine mwaka 2014 imekuwa ikilengwa katika mashambulio ya hivi karibuni tangu rais wa Urusi Vladimir
Putin alipoamuru wanajeshi wake waivamie kikamilifu Ukraine mwezi Februari mwaka 2022. 

Moja ya zana ya kivita inayotumiwa na vikosi vya Urusi huko Mashariki mwa Ukraine
Moja ya zana ya kivita inayotumiwa na vikosi vya Urusi huko Mashariki mwa UkrainePicha: Russian Defence Ministry/dpa/picture alliance

Kando na hilo msemaji wa kundi la kijeshi la upande wa mashariki mwa Ukraine amesema kundi la mamluki wa kampuni binafsi ya kijeshi kutoka Urusi ya Wagner, limerejea tena mashariki mwa taifa hilo. 

Jeshi hilo limesema baada ya wanachama wa Wagner kwenda barani Afrika baadhi yao walibakia na kusaini mikataba mipya  na wizara ya ulinzi ya Urusi na kwa sasa wanashiriki katika operesheni za kijeshi upande huo wa Mashariki.

Soma pia:Ukraine imesema makamada wa jeshi wa Urusi wameuwawa Crimea

Hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti wapiganaji wa Wagner kujihusisha na mapigano karibu na mji wa Bakhmut.

Wakati hayo yakiarifiwa waziri wa kilimo wa Poland Robert Telus amesema nchi yakeimeingia katika mazungumzo na Ukraine baada ya nchi hizo mbili kuingia katika mvutano juu ya uamuzi wa serikali mjini Warsaw wa kurefusha marufuku ya usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia ardhi ya Poland. 

Telus ameyasifu mazungumzo hayo akiyataja kuwa njia muhimu ya kutatua tofauti zilizojitokeza kati ya nchi hizo mbili.