1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Marekani zasaini mkataba wa START

Saumu Ramadhani Yusuf8 Aprili 2010

Mkataba huo umeidhinishwa na pande zote mbili kwa dhamira ya kupunguza silaha za Nuklia katika nchi hizo

https://p.dw.com/p/MqB7
Rais Barack Obama, na Dmitry MedvedevPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama na mwenzake wa Urusi Dmitry Medvedev wamekutana mjini Prague huko  jamhuri ya Czech  hii leo kwa ajili ya kutia saini mkataba mpya wa upunguzaji silaha unaofahamika kama START.Mkataba huo  utachukua mahala pa ule uliomalizika muda wake uliofikiwa mwaka 1991.

Viongozi hao wawili wamejiandaa kutia saini makubaliano ya pamoja kuhusu suala la kupunguza silaha za Kinuklia katika mataifa yote mawili.Kabla ya sherehe ya kusainiwa mkataba huo mpya wa Start marais Barack Obama na Dmitry Medvedev  walikuwa na mazungumzo ya pamoja ya kina kuhusiana na masuala mbali mbali.

Rais Obama alishazungumzia juu ya malengo yake na matarajio ya kuondoa kabisa silaha za Nuklia duniani kiasi mwaka mmoja  uliopita katika wakati akifanya ziara katika mji mkuu huo wa jamhuri ya Czech. Rais Obama amesisitiza kwamba ni  suala muhimu kwa Marekani na jumuiya nzima kwa jumla ya kimataifa kutia juhudi katika kuzuia kabisa matumizi ya silaha za Nuklia.

Atomwaffenfähige Rakete, Atomwaffe
Picha: AP

Marekani na Urusi zinamiliki kiasi asilimia 90 ya sialaha za Nuklia duniani na viongozi wa nchi hizo mbili wamesema kwamba mkataba huo wa START  utakuwa ni mfano kwa nchi zingine ambazo zina silaha za Nuklia au zinanuia kuwa nazo.Baada ya kuwasili mjini Prague  hapo jana rais wa Urussi Dmitry Medvedev  aliutaja mkataba huo mpya wa kupunguza silaha za maangamizi makubwa,kuwa ni muhimu sana  ambao utachangia katika kuanzishwa juhudi za kimataifa za kuondoa kumaliza kabisa silaha za Nuklia.

Chini ya mkataba huo nchi hizo mbili  zitawajibika kupunguza sialaha 1,550 kila mmoja au kiasi cha thuluthi moja chini ya viwango vyake vya sasa.Silaha hizo ni pamoja na nyambizi pamoja na mabomu yenye nguvu kubwa.

Hata hivyo kuna wanaoukosoa mkataba huo ambao wanautaja kama ni wa wastani sana ambao haujazingatia mambo mengi muhimu na pia haujakwenda umbali wa kutosha kuzitia motisha  nchi zingine kuachana na silaha hizo za maangamizi makubwa.

Kwa upande mwingine malengo ya rais Obama ya kutaka ulimwengu uishi bila ya kuwa na silaha za Nuklia,yataingia katika mtihani wake wa kwanza hivi karibuni kwani makubaliano ya Start yanatiwa saini wakati ambapo wiki ijayo kutakuwa na mkutano wa kilele mjini Washington  juu ya usalama wa Nuklia  kuanzia tarehe 12 hadi 13.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE 

Mhariri AbdulRahman