Urusi na Ukraine zashambuliana kwa makombora na droni
25 Novemba 2024Urusi imefanya mashambulio kadhaa katika maeneo mbali mbali ya Ukraine ikiwa ni pamoja na Kharkiv ambako watu wasiopungua 10 wamejeruhiwa leo asubuhi.
Gavana wa jimbo hilo Oleh Syniehubov amesema moto mkubwa ulisababishwa na shambulio hilo katika mitaa ya katikati ya mji na kuharibu majengo ya raia pamoja na magari.
Vikosi vya Urusi vimeshambulia pia miundo mbinu ya nishati katika eneo la Kusini mwa Ukraine la Mykolaiv pamoja na miundo mbinu ya viwanda katika jimbo la Kusini mashariki la Zaphorizhizhia usiku wa kuamkia leo.
Mifumo ya ulinzi ya Ukraine ilifanikiwa kuziangusha droni mbili kwenye eneo hilo huku ikiripotiwa kwamba hakuna wahanga wa shambulio hilo japo imeleezwa kwamba makumi ya droni za Urusi zilishambulia Zaporizhizhia.
Mfumo wa ulinzi pia ulizuia shambulia la droni katika mji mkuu Kiev na maeneo mengine yanayozunguka eneo hilo usiku wa kuamkia leo.
Rais Volodymyr Zelensky jana Jumapili alisema Urusi imetumia kiasi droni 460 na zaidi ya makombora 20 kuishambulia Ukraine katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Ripoti zinasema nayo Ukraine imefyetuwa makombora saba na droni kuelekea Urusi lakini yalidunguliwa usiku wa kuamkia leo katika eneo la Kursk upande wa Urusi.
Wachambuzi wameyaita mashambulio hayo ya Ukraine kuwa makubwa kabisa katika ardhi ya Urusi yakitumika makombora ya mataifa ya kigeni.
Wizara ya ulinzi ya Urusi asubuhi ya leo Jumatatu imesema jumla ya droni 23 za Ukraine zilidunguliwa katika anga ya Urusi,lakini taarifa ya wizara hiyo haikutaja chochote kuhusu mashambulizi ya makombora kutoka Ukraine.
Wakati huohuo ripoti zinasema kwamba jeshi la Urusi limemkamata raia mmoja wa Uingereza aliyekuwa vitani bega kwa bega akivisaidia vikosi vya Ukraine katika jimbo la Kursk lililonyakuliwa kwa muda na Urusi.
Shirika la habari la Tass limesema mpiganaji huyo ametambuliwa kwa jina la James Scott Rhys Anderson.
Imeripotiwa kwamba Anderson alikuwa mkufunzi wa vikosi vya Ukraine na alipelekwa katika jimbo la Kursk kinyume na ridhaa yake.
Wasiwasi wa Kimataifa waongezeka
Vita hivi vya Ukraine hivi sasa vimeibuwa wasiwasi mkubwa katika Jumuiya ya Kimataifa,mawaziri wa ulinzi kutoka hapa Ujerumani,Ufaransa,Poland,Italy na Uingereza wanajiandaa kukutana kujadili hatua za kuimarisha usalama na ulinzi Ulaya.
Na kwa upande mwingine katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikosoa hatua ya Marekani ya kutaka kuipatia Ukraine mabomu ya kutega ardhini, akiita hatua hiyo ni kitisho kipya.
Kauli ya Guterres imetolewa kwenye mkutano unaofanyika Cambodia wa kutathmini hatua zilizopigwa kwenye mkataba wa kuzuia mabomu ya kutega ardhini duniani.
Guterres pamoja na kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis na viongozi wengine wametowa mwito wa kuzuia utengenezaji na matumizi ya mabomu hayo.