1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaizuia ndege ya Ujerumani kujaza mafuta Moscow

1 Februari 2020

Ndege ya kijeshi ya Ujerumani iliyokuwa imewapakia raia walioondolewa China kutokana na virusi vya Corona imezuiwa kujaza mafuta nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/3X8cd
Deutschland Coronavirus Rückholungsflug
Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 128 walioondolewa Wuhan, mji ambako virusi hivyo vilianzia, ilikuwa ikitarajiwa kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Frankfurt Jumamosi asubuhi, lakini ilichelewa kutokana na masuala yaliyojitokeza kati ya Ujerumani na Urusi.

Nchi mbalimbali duniani zimekuwa zikichukua hatua za kuwalinda raia wake wakati visa vya virusi vya Corona vikiongezeka.

Ndege hiyo aina ya Airbus A310 ilikuwa isimame mjini Moscow kwa ajili ya kubadilisha wafanyakazi pamoja na kujaza mafuta.

Hata hivyo, Urusi ilikataa kuiruhusu ndege hiyo kutua kutokana na uwanja wa Moscow kutokuwa na uwezo wa kuiruhusu ndege hiyo kutua na badala yake ilibadili njia na kuelekea Helsinki, Finland.

Afisa katika wizara ya afya ya Ujerumani amesema ndege hiyo ina raia 110 wa Ujerumani. Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, DPA, madaktari pia wamo ndani ya ndege hiyo kwa ajili ya kuwaangalia abiria.

Frankfurt Flughafen Quarantänehalle für Corona-Evakuierte
Eneo la karantini ambako watawekwa raia wa Ujerumani waliorudishwa kutoka ChinaPicha: Getty Images/AFP/Y. Schreiber

Raia hao watawekwa katika karantini kwenye kambi ya jeshi iliyo karibu na uwanja wa ndege wa Frankfurt. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema hakuna raia yeyote wa Ujerumani kati ya wanaorudishwa nchini anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema ndege hiyo ilipeleka msaada kwa maafisa wa China katika jimbo la Wuhan ambalo linapambana na virusi hivyo, zikiwemo nguo maalum 10,000 za kujikinga ambazo China waliomba.

Hadi sasa Ujerumani imethibitisha kuwepo wagonjwa saba wa virusi vya Corona na nchi hiyo imewashauri wananchi wake kujizuia kwenda China iwapo safari zao sio za lazima.

Dharura ya kimataifa

Siku ya Alhamisi Shirika la Afya Duniani, WHO lilivitangaza virusi vya Corona kuwa dharura ya kimataifa. Idadi ya watu duniani walioambukizwa ugonjwa huo inakaribia 12,000, huku visa vingi vikiwa ni kutoka China. Siku ya Jumamosi maafisa wa China wamesema idadi ya vifo vilivyotokana na virusi hivyo nchini humo imefikia 259.

Hadi sasa idadi ya watu walioambukizwa kirusi cha Corona imepanda na kufikia visa 11,791 ikiipiku idadi ya watu waliokumbwa na mripuko wa maradhi ya SARS mwaka 2002-2003.

Nje ya China zaidi ya watu 120 wameambukizwa virusi hivyo katika nchi mbalimbali. Kwa mujibu wa takwimu za WHO nchi zilizoathirika mbali na China ni pamoja na Thailand, Japan, Singapore, Korea Kusini, Taiwan, Malaysia, Australia, Ujerumani, Marekani, Ufaransa na Vietnam.

Nchi nyingine ni Canada, Urusi, Italia, Uingereza, Cambodia, Finland, India, Ufilipino, Nepal, Sri Lanka, Sweden, Uhispania pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Schweiz Genf | Pressekonferenz  WHO - Tedros Adhanom Ghebreyesus Ruft Gesundheitsnotstand wegen Coronavirus  aus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: picture-alliance/KEYSTONE/J.-C. Bott

Wakati huo huo, China imetangaza kuwa bidhaa za Marekani ambazo zinaweza kutumika katika kukabiliana na virusi hatari vya Corona zitaondolewa ushuru.

Uamuzi huo umetolewa wakati ambapo China inapambana kuvidhibiti virusi hivyo vilivyosababisha uhaba wa vifaa vya tiba kwenye mji wa Wuhan ambao umeathirika zaidi.

China na Marekani zimekuwa katika vita ya kibiashara kwa karibu miaka miwili, ingawa pande zote mbili zilifikia makubaliano kuondoa ushuru huo mwezi uliopita, huku China ikikubali kununua bidhaa zenye thamani ya Dola bilioni 200 kama sehemu ya makubaliano hayo ya kibiashara.

Huku hayo yakijiri, mashirika mbalimbali ya ndege duniani yameendelea kusitisha safari zake kwenda China kutoka na mripuko wa virusi vya Corona. Nchi ambazo mashirika yake ya ndege yamesimamisha safari ni pamoja na Canada, Ufaransa, India, New Zealand, Vietnam, Tanzania, Uturuki, Korea Kusini, Turkmenistan, Marekani, Kenya na Uingereza.

Nchi nyingine ni Misri, Israel, Ethiopia, Finland, Indonesia, Poland, Ujerumani, Australia, Qatar, Morocco, Urusi, Rwanda, Singapore pamoja na miji ya Abu Dhabi na Hong Kong.

(AP, AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2vGQwTX)