Ushindi wa Tshisekedi wapokelewa kwa shangwe
10 Januari 2019Kwa upande wake, Martin Fayulu, mgombea mwingine wa upinzani, amepinga matokeo hayo na kusema hayakubaliki hata kidogo. Wafuasi wa UDPS waliripuka kwa shangwe kishangilia ushindi wa Felix Tshsekedi mara tu alipotangazwa kuwa rais mteule wa Congo. Tshisekedi amesema kwamba ushindi huo ni wa raia wa Kongo na atakuwa rais wa wakongomani wote:
"Nitakuwa rais wa wakongamani walionichaguwa na wale ambao hawakunichaguwa, sitokuwa rais wa kundi la watu, au wachama fulani au wa kabila Fulani.Nitakuwa rais wa Wacongamani wote wa kike na wakiume,” alisema Tshisekedi .
Mgombea kiti cha rais wa mungano wa Lamuka , Martin Fayulu ametangaza kwamba anapinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaliyotangazwa alfajiri ya alhamisi na tume huru ya uchaguzi CENI.
Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi habari baada ya kutangazwa kwa matokeo ya awali, Fayulu amesema matokeo hayo yametungwa, yamepangwa na hayakubaliki kamwe.
"Hatuezi kukubali baada ya njia ndefu ya msalaba kwamba matakwa ya raia wetu yasitekelezwe.Ndio kwa maana sisi wote kwa pamoja tupinge uongo wa Corneille Nangaa mwenye kiti wa CENI na kupangwa kwa matokeo ya uchaguzi”.
Nangaa anasema hivi sasa matokeo hayo yatawasilishwa mbele ya mahakama ya katiba ambayo ina siku 7 za kusikiliza malalamiko kabla ya kuchapisha matokeo rasmi siku mbili baadae.
Wachambuzi wanasema matokeo hayo bila shaka yatapatia nguvu tetesi kwamba Tshisekedi ambae alikua nyuma sana ya Fayulu katika uchunguzi wa maoni ya watu kabla ya uchaguzi, alifikia makubaliano ya kugawana madaraka na rais Kabila.
Fayulu ambae amepata karibu kura milioni 6 amesema hatakubali kuibiwa kura kama walivyoibiwa Jean Pierre Bemba mwaka 2006 na Etienne Tshisekedi 2011, akitoa wito kwa Baraza la kidini kumtangaza mshindi wa kweli wa ucahguzi huo.
Mgombea wa muungano unaotawala wa FCC, Emmanuel Shadari anatarajiwa kutangaza msimamo wake hivi karibuni.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo
Mhariri: Iddi Ssessanga