Wake zake wawili waliaga dunia, hivyo kusalia na wake 10. Heshima na utulivu umewasaidia kuishi kwa amani katika boma hili kubwa. Kifunguamimba wake Morijoi Naurori ambaye hataki kufichua mengi kuhusu ugonjwa wa mzee anasema hatawahi kusahau hadithi aliyotambiwa na baba yake. Katika ujana wake, mzee alikuwa anaiba mifugo katika taifa jirani la Tanzania, ambapo alikamatwa na kufungwa kwa miaka saba.
Kutunza na kuishi na wake wengi sio kazi lelemama. Mzee Naurori, amewajengea wake zake nyumba zao. Ili kufaulu, kuwalisha na kukimu mahitaji yao, anakiri kuwa utajiri wake umemfaa. Mzee anamiliki zaidi ya ng'ombe 1000, kondoo na mbuzi 5000, ambao mara nyingi huwachinja kwa mlo. Kwa mujibu wa baadhi ya wanafamilia hapa, mifugo hawa, hulishwa katika shamba lake kubwa. Mzee huhofia kuvamiwa kwa mifugo wake wakiondoka nje ya boma. Kila familia huwa na zamu ya kuwachunga mifugo.