Uwazi katika mapambano ya usafirishaji haramu wa dhahabu nchini Kongo
Uwazi kwenye biashara ya dhahabu ni njia mpya inayotumika nchini Kongo, kwa kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kuangazia biashara ya dhahabu
Kwa kawaida, dhahabu nyingi inayochimbwa mashariki mwa Kongo husafirishwa kimagendo hadi Rwanda. Primera Gold, mradi unaoendeshwa kwa ubia kati ya Kongo na Umoja wa Falme za Kiarabu, unalenga kufanya biashara ya dhahabu kwa uwazi.
Biashara halali sio magendo
Kulingana na Benjamin Bisimwa, kaimu mkurugenzi mkuu wa Primera Gold, karibu tani moja ya dhahabu huvuka mpaka kinyume cha sheria kila mwezi ni kilo 34 pekee (takriban pauni 75) ambazo zilitangazwa rasmi kuuzwa nje ya nchi mwaka 2022. Ndani ya miezi kadhaa baada ya kuzindua shughuli zake, Primera Gold ilisafirisha rasmi tani 1 ya dhahabu.
Dhahabu ya majimaji
Mfanyikazi huyu anamimina dhahabu ya majimaji kwenye chombo. Dhahabu ina uzito wa takribani kilo 2 na thamani yake ni zaidi ya €110,000 (takriban $117,000). Kifaa cha kupima kimethibitisha usafi wa asilimia 96.8, wa dhahabu hiyo ambayo ni miongoni mwa dhahabu safi zaidi ulimwenguni kulingana na wataalam wa tasnia.
Kazi ya hatari
Primera Gold imesema inataka kuboresha mazingira ya kazi kwa wachimbaji migodi. Wazo pia ni kuwapa bima ya afya, lingawa hadi sasa mafanikio bado ni madogo. Wachimbaji wanaendelea kufanya kazi katika mazingira hatari bila vifaa vya vya usalama vinavyoridhisha, wakati mwingine wanatembea bila viatu.
Je matatizo ya wachimbaji yatapunguzwa?
Matarajio ya kampuni hiyo nchini Kongo yanaungwa mkono, lakini pia kuna mashaka. Blaise Bubala, mwakilishi wa mashirika ya kiraia wa kanda hiyo, amesema "bado kuna utata." Ingawa serikali inamiliki asilimia 45 ya kampuni ya Primera Gold, kuna shaka iwapo fedha zitawanufaisha jamii maskini ambazo hazina shule, barabara na hospitali.
Siku za usoni bila uhakika
Kampuni ya Primera Gold imekiri kuwa bado ina safari ndefu kuhusiana na usalama wa wachimbaji migodi, lakini msemaji wa kampuni hiyo Bisimwa ameahidi kuwa changamoto zitatatuliwa kwa pamoja. Ishara chanya: msako mkubwa wa uuzaji haramu wa dhahabu katika eneo hilo tarehe 1 Mei.