1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

VIENNA : Wakaguzi wa nuklea kuzuru Korea Kaskazini

23 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBpI

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la masuala ya nuklea la Umoja wa Mataifa Mohamed El Baradei amesema wakaguzi wa nuklea wa Umoja wa Mataifa watawasili nchini Korea Kaskazini hapo Jumanne kuanza mazungumzo juu ya kuufunga mtambo wa nuklea wa Yongbyon.

Mtambo huo ni kitovu cha mpango wa nuklea wa Korea Kaskazini.Ziara hiyo inafuatia mwaliko kutoka serikali ya nchi hiyo na itakuwa ni ziara ya kwanza kufanywa na wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomu karibu katika kipindi cha miaka mitano baada ya kutimuliwa na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Il mwishoni mwa mwaka 2002.

Hapo awali Msaidizi waziri wa mambo ya nje wa Marekani Christopher Hill amesema utawala wa Kim ulikuwa tayari kuufunga mtambo huo wa Yangbyon.

Kuukongowa mtambo huo ni mojawapo ya vifungu vya makubaliano yaliofikiwa katika mazungumzo ya pande sita juu ya mzozo wa nuklea wa Korea Kaskazini mapema mwaka huu.

Wakati huo huo imefahamika kwamba msluhishi mkuu wa masuala ya nuklea wa Iran Ali Larijani amekubali kuandaa mpango wa kufanyiwa kazi juu ya namna ya kuutauwa mzozo wa nuklea wa Iran katika kipindi kisichozidi miezi miwili.

El Baradei ameuelezea mkutano wake wa Ijumaa na Larijani kuwa wa kuridhisha.