Vikosi vya DRC vyakumbana na mashambulizi
17 Septemba 2018Vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimekabiliwa na mashambulizi makali kutoka kwa waasi wa nchi hiyo katika jimbo la Kivu Kusini.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kijeshi na raia, jana Jumapili vikosi vya jeshi la Kongo vilikabiliana na muungano wa waasi wa Yakutumba, ambao unamtii mkuu wa zamani wa jeshi, ambaye anampinga Rais Joseph Kabila pamoja na washirika wake wa Malaika.
Vyanzo hivyo vilivyozungumza kwa sharti la kutotambulishwa, vimesema waasi wameviteka vijiji vitatu katika mkoa wa Fizi, uliopo kusini katika jimbo lenye utajiri wa madini linaloelekea kutumbukia katika mvutano wa kikabila.
Msemaji wa jeshi amethibitisha taarifa hizo kwa shirika la habari la AFP. Mwezi Januari, jeshi lilisema kwamba limewaondoa waasi wa Yakutumba kwa msaada wa nchi jirani ya Burundi, ambako baadhi ya waasi hao wameomba hifadhi.