1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wajadili mageuzi kwenye AU

17 Novemba 2018

Viongozi wa nchi na mawaziri kutoka nchi 55 wa Umoja wa Afrika wanakutana katika kile kinachoonekana juhudi za dakika ya mwisho za kufikia makubaliano kuhusu haja ya kuufanyia Umoja wa Afrika mageuzi.

https://p.dw.com/p/38R20
Äthiopien Addis Abeba Afrikanische Union Gipfel
Picha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Rais wa Rwanda Paul Kagame amewahimiza viongozi wenzake wa nchi za Afrika kufikia makubaliano kuhusu maguezi yaliyojadiliwa kwa muda mrefu kuhusu Umoja wa Afrika. Kagame ameyasema hayo katika mkutano maalumu wa kilele wa Umoja huo unaofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Je, mageuzi yatafikiwa?

Viongozi wa nchi na mawaziri kutoka nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya Umoja huo katika kile kinachoonekana juhudi za dakika ya mwisho za kufikia makubaliano kuhusu haja ya kuufanyia Umoja wa Afrika mageuzi, mazungumzo ambayo yamedumu kwa takriban miaka miwili.

Ruanda Kigali Unterzeichnung Afrikanisches Freihandelsabkommen
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Imago/Xinhua/G. Dusabe

Kagame ambaye ni mwenyekiti wa Umoja huo amesema kuna haja ya dharura ya kutekeleza maguezi katika umoja huo ambao mara nyingi unaonekana kutokuwa na nguvu na unaotegemea pakubwa misaada kutoka kwa wafadhili.

Akiufungua mkutano huo maalumu wa kilele, Rais huyo wa Rwanda amesema matukio barani Afrika na kwingineko duniani yanathibitisha umuhimu na haja ya dharura ya kutekeleza mabadiliko kwa lengo la kuifanya Afrika imara zaidi na kuwapa watu wake mustakabali unaostahili wa siku za usoni.

Muhula wa Kagame wa kuhudumu kama mwenyekiti wa Umoja wa Afrika unakamilika mwezi Januari na wachambuzi wanasema muda unayoyoma kwa kiongozi huyo kutekeleza mpango wake wa kuleta mageuzi katika umoja huo huku Misri ikitarajiwa kuchukua uenyekiti huo mwaka ujao na ikiwa haina urari wa kuendeleza ndoto hiyo ya kuleta mageuzi.

Kwenye mapendekezo yaliyozinduliwa mwaka jana, Kagame alinuia kufikia halmashauri yenye mamlaka zaidi iliyo na maafisa wachache ambayo gharama zake zitagharamiwa na nchi wanachama badala ya wafadhili wa nchi za kigeni. Lakini nchi kubwa za Afrika zina mashaka na halmashauri yenye nguvu kubwa inazoamini itaingilia uhuru wa nchi hizo za kujitawala zinavyotaka.

Kiongozi wa Ethiopia asifiwa

Kagame alipendekeza pia nchi wanachama wamchague mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika ambaye atakuwa na mamlaka ya kumteua naibu wake na makamishna wa halmashauri hiyo, pendekezo ambalo lilikataliwa na viongozi.

Äthiopien Abiy Ahmed Premierminister
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: picture-alliance/AP Photo/Saudi Press Agency

Pia alitaka kupunguza majukumu ya Umoja wa Afrika kutuama katika nyanja nne ambazo ni amani na usalama, utangamano wa kiuchumi, masuala ya kisiasa na uwakilishi wa Afrika katika safu ya kimataifa.

Viongozi wa Afrika wamemsifu waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kwa kuleta mageuzi makubwa nchini mwake.

Abiy mwenye umri wa miaka 42 amewaeleza viongozi wa Afrika wanaokutana katika mkutano maalumu wa kilele kuhusu Umoja wa Afrika kuhusu mageuzi aliyoyafanya tangu alipoingia madarakani mwezi Aprili mwaka huu.

Miongoni mwa mageuzi hayo ni kuwaachia huru maelfu ya wafungwa, kuviondolea marufuku vyama vya kisiasa, mashirika ya habari na mitandao, kuleta maridhiano na kupambana na ufisadi.

Waziri huyo mkuu wa Ethiopia amewahimiza viongozi wengine wa Afrika kufanya mageuzi makubwa ili kupiga hatua katika amani na maendeleo barani Afrika.

Mwandishi: Caro Robi/AFP/AP

Mhariri: Lilian Mtono