1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wana wasiwasi na hali ya DRC

Admin.WagnerD27 Desemba 2018

Viongozi wa nchi za Afrika wameelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya visa vya vurugu na ukatili wakati wa kampeni za urais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo siku chache kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika nchini humo.

https://p.dw.com/p/3Ag2v
Democratic Republic of the Congo Demonstration in Goma Kongo Lucha
Picha: picture-alliance/AA/JC Wnga

Viongozi hao kutoka Angola, Botswana, Congo, Namibia, Rwanda, Afrika ya kusini, Uganda na Zambia ambao walikutana jana mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazzaville, wamesema kwenye taarifa ya pamoja kuwa makabiliano kwenye baadhi ya maeneo wakati wa kampeni Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yanaweza kuwavunja moyo wapiga kura.

Mkutano huo wa siku moja ambao uliitishwa kujadili hali ya Congo kuelekea uchaguzi mkuu wa Jumapili ijayo, uliwaleta pamoja viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya maendeleo ya kiuchumi kusini mwa Afrika SADC na wale kutoka jumuiya ya nchi za maziwa makuu.

Hakuna mjumbe kutoka Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo aliyehudhuria mkutano huo lakini viongozi hao wamekubaliana kutuma ujumbe wa mawaziri wa mambo ya kigeni kwenda Kinshasa kuwasilisha maazimio ya mkutano wa Brazzaville kwa rais Joseph Kabila.

Mkutano huo umefanyika siku tatu kabla ya kufanyika uchaguzi nchini Congo na viongozi hao walilenga kutathmini hali ya ulinzi na amani kusini mwa jangwa la sahara na mchakato wa uchaguzi katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.

Wakongomani wanatafuta hifadhi.

Kongo Flüchtlinge
Picha: picture-alliance/dpa

Jamhuri ya Congo ambayo inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tayari inakabiliana na wimbi la wakongomani wanaopindukia 15000 ambao wanaishi kwenye mpaka w anchi hizo mbili wakihofia hali ya usalama ndani ya Congo kuelekea uchaguzi.

Shirika la kuwahudimia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema hivi karibuni kuwa kiasi ya  wakongomani laki saba na nusu wameikimbia nchi yao wakijaribu kutafuta hifadhi katika nchi jirani.

Kulingana na duru za kuaminika watu kadhaa wameshapoteza maisha katika machufuko ya wakati wa kampeni za uchaguzi madai ambayo hata hivyo serikali ya Congo imekanusha.

Mgombea wa urais wa upinzani Martin Fayulu amenukuliwa akidai kuwa alizuiliwa kuitembelea miji ya, Kindu, Kolwezi na Kinshasa, wakati wa kampeni.

Mrithi wa rais Kabila atapatikana?

Uchaguzi wa Congo unalenga kumpata mrithi wa rais Joseph Kabila ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miongo miwili.

DRC Präsident Joseph Kabila
Picha: Reuters/K. Katombe

Rais Kabila alipaswa kumaliza muhula wake mamlakani mnamo mwaka 2016 lakini amesalia madarakani baada ya kutengua ibara ya katiba inayoweka marufuku hiyo.

Uchaguzi mkuu uliahirishwa hadi mwishoni mwaka 2017 baada ya kanisa katoliki kufanikisha makubaliano, lakini uliaharishwa tena hadi 2018 na rais kabila alitangaza kutowania kwenye uchaguzi huo.

Wiki iliyopita tume ya uchaguzi ilisogeza mbele tarehe ya kupiga kura kwa muda wa wiki moja kutokana na moto ulizuka kwenye ghala la vifaa vya uchaguzi mjini Kinshasa kutatiza uwezekano wa zoezi hilo kufanyika.

Hata hivyo wasiwasi bado ni mkubwa kuelekea uchaguzi wa jumapili baada ya hapo jana tume ya uchaguzi kutangaza kuwa upigaji kura hautofanyika kwenye majimbo ya Beni Butembo na Yumbi kwa sabau ya homa ya ebola na kitisho cha ugaidi.

Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP

Mhariri: Josephat Charo