Viongozi wa mataifa ya Ulaya na NATO kuijadili Ukraine
18 Desemba 2024Mkutano huo wa viongozi unaowajumuisha wale wa Ufaransa, Ujerumani na Poland pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya nchi za magharibi, NATO, unafanyika katikati ya miito kutoka Ukraine, ikiwataka washirika wake kuipiga jeki kwenye uwanja wa vita na kidiplomasia kabla ya uwezekano wa kufanyika mazungumzo yoyote na Urusi.
Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine tayari yuko mjini Brussels kushiriki mkutano huo na ameashiria kwamba suala la kupelekwa wanajeshi kigeni nchini mwake linaweza kuwa moja ya masuala yatakayojadiliwa. Zelensky amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk.
Uwezekano huo wa kutumwa wanajeshi wa kigeni nchini Ukraine ulitajwa kwa mara ya kwanza na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa mnamo mwezi Februari lakini hadi sasa bado hakuna mwafaka miongoni mwa viongozi wa mataifa ya Ulaya juu ya suala hilo.