Viongozi wa Urusi na Iran wasaini mkataba wa ushirikiano
17 Januari 2025Matangazo
Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Iran Masoud Pezeshkian wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakatikatika Ikulu ya Kremlin Ijumaa, yanayolenga kuimarisha ushirikiano, katikati ya machungu ya vikwazo vya magharibi.
Kulingana na Kremlin, makubaliano hayo ya ushirikiano wa kina na kimkakati yatagusa maeneo yote kuanzia biashara na kijeshi hadi sayansi, elimu na utamaduni.
Ziara hiyo ya Pezeshkian inafanyika siku chache kabla ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, aliyeahidi kusimamia usitishwaji wa vita nchini Ukraine na kuchukua msimamo mkali dhidi ya Iran.
Mwanzoni mwa mazungumzo yao, Putin amemwambia Pezeshkian kwamba makubaliano hayo mapya yatatoa msukumo wa ziada kwenye karibu maeneo yote wanayoshirikiana.